JAMHURI imedai kuwa Marekani ilianza kumchunguza Kiongozi wa Taasisi ya Kusafirisha na Kusambaza Dawa za Kulevya Tanzania, Ally Haji na wenzake kwa miaka minne na walitumia Dola za Marekani 10,000 (zaidi ya Sh milioni 22) kununua dawa hizo ili kuwachunguza.
Wakili Majura Magafu amedai kuwa aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, alikosea kupokea maombi ya kuwasafirisha Watanzania kwenda Marekani, hakuwa makini kusoma nyaraka zao kwani angesoma angebaini upungufu na hivyo angewabishia Wamarekani na kuyakataa maombi yao.
Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki alipowasilisha maombi na ushahidi dhidi ya wajibu maombi.
Dk. Mwakyembe aliwasilisha maombi Februari 15 mwaka huu, akiomba mahakama hiyo kuamuru Watanzania watatu akiwamo Ally Haji, maarufu Shikuba kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kakolaki alidai wajibu maombi Ally Haji au Ally Hassan, maarufu Shikuba, Iddy Mfuru na Tiko Adam walikula njama kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini Marekani.
“Wajibu maombi ilibainika walikuwa wakisafirisha heroine kwa kutumia magari binafsi, wakifikisha Marekani wanawatumia watu kusambaza kwa kutumia ndege binafsi na Shikuba ndiye kiongozi wa taasisi hiyo,”alidai.
Kakolaki alidai maombi hayo yaliyowasilishwa mahakamani ya kutaka wajibu maombi wapelekwe Marekani yaliambatanishwa na kiapo kilichoapwa na Richard Mangnes ambaye katika kiapo chake anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.
Alidai ushahidi katika kiapo hicho unadai aliwahi kukamatwa mbeba dawa (punda) mwaka 2012, alizitoa kwa njia ya haja kubwa na alipohojiwa alimtaja Shikuba kuwa alimpa dawa hizo.
Kakolaki alidai tangu mwaka 2005 wajibu maombi wanatajwa na watuhumiwa mbalimbali nchini Marekani kwamba ndio wanaosambaza dawa hizo kwa kutumia taasisi yao inayoongozwa na Shikuba.
Katika ushahidi huo wa kiapo unadai Shikuba aliwafundisha miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa jinsi ya kubeba dawa hizo na kusafirisha na kwamba dawa hizo zilikuwa zikiingia Tanzania kwa meli kupitia mwambao wa Tanzania kwa maelekezo ya Shikuba.
“Msambazaji mmoja alikutana na Shikuba Dubai, akamlipa Dola za Marekani 50,000 (zaidi ya Sh milioni 250) kwa ajili ya kusambaza dawa za kulevya kilo 100, fedha zingine walikubaliana kulipana baada ya kazi.
Kuhusu Mfuri alidai Wakala maalum aitwaye, Mathew alimfuatilia na kubaini kwamba ni mwanachama katika taasisi hiyo na kwamba anasafirisha dawa hizo pia.
Inadaiwa mmoja wa wasambazaji alikubaliana na Mfuru kununua kilo 10 za heroine.
Mathew anadai katika kiapo chake kwamba Mfuru alimkodi mtu mwingine kupokea dawa hizo maeneo ya Mwambao wa Bahari ya Tanzania.
Alidai katika kufanya uchunguzi Mathew alijifanya mnunuzi anahitaji kilo 10 katika taasisi hiyo na alizungumza kwa simu na Mfuru ili kupata mzigo huo wa dawa.
Mfuru alimtambulisha rafiki yake ambaye ni kiongozi wa taasisi hiyo ambaye ni Shikuba kwa mteja na wakiendelea kuwasilisna alimtumia namba ya mshiriki mwenzake Tiko Adam aliyekuwepo Afrika Kusini ili mteja ampigie simu kwa ajili ya kupata mzigo.
Mteja aliwasiliana na Tiko na mzigo ulifika Marekani, Novemba 29 mwaka 2013 walifanya mazungumzo kati ya Tiko na mteja wakakubaliana kukutana hotelini ambapo walikutana.
0 Post a Comment:
Post a Comment