Mkwasa aipiga kijembe Simba



 Katibu wa Yanga, Charles Mkwasa ametia chumvi kwenye kidonda baada ya kuwataka watani zao Simba kucheza mpira uwanjani badala ya kukimbilia mezani kudai pointi.
Baada ya kupokwa pointi hizo Simba sasa inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 59, ikifuatiwa na Yanga (56) yenye michezo miwili mkononi.
Kauli hiyo ya Mkwasa imekuja siku moja baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka Simba pointi ilizopewa na Kamati ya Saa 72 na kuzirejesha kwa Kagera Sugar iliyodaiwa kumchezesha Mohammed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Akizungumza katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika makao makuu ya klabu ya Yanga, Mkwasa alisema umefika wakati klabu zicheze mpira uwanjani.
"Sitaki kuitaja timu gani, lakini natoa kama angalizo, hizi kanuni ziangaliwe. Hata kama mchezaji akiwa na kadi suluhu siyo kuinyang'anya ushindi bali kumwadhibu mchezaji husika, tuziangalie kanuni hizi," alisema Mkwasa.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alisema kila kitu kinakwenda sawa katika kikosi chao na masuala ya nje ya uwanja wameyaacha kwa uongozi na akili za wachezaji ni mechi zilizosalia za Ligi Kuu na Kombe la FA.
"Mambo ya nje ya uwanja hayatuhusu, kuna mahala pake na wachezaji wanachokifikiria ni matokeo ya uwanjani hivi sasa, timu hiko sawa na hayo yaliyotokea tumeuachia uongozi ushughulike nayo, hayajaivuruga timu na wala hayatuzuii kushinda mechi zetu zilizosalia," alisisitiza Mgosi.
 Mchambuzi Jeff Leah alisema tofauti ya pointi na Yanga ni tatu, lakini Yanga ina michezo miwili mkononi, kitu ambacho kinaipa Simba wakati mgumu kutwaa ubingwa, labda itokee bahati ya mtende.
"Kwangu mimi naona labda ielekeze nguvu katika Kombe la FA na ifuzu kucheza fainali hapo itakuwa imefufua matumaini ya kushiriki mashindano ya kimataifa, lakini kwenye ligi itachukua taji hilo kwa bahati.
Ally Mayay alisema bado anaamini nafasi ya ubingwa ipo wazi kwa Simba kama akifanikiwa kushinda mchezo dhidi ya African Lyon.
"Kitu ambacho unacho mkononi ni bora kuliko ambacho huna, Yanga haijapata bado pointi ingawa ina michezo miwili mkononi, tofauti na Simba ambayo ina pointi, lolote linaweza kutokea kwa Yanga hasa kwenye mechi dhidi ya Mbao na Toto ambazo ziko katika hatihati ya kushuka daraja.
"Kinachotakiwa ni Simba kutulia na kushinda mchezo wa Lyon ambayo ina nyota wengi walioichezea Simba, kama ikifanikiwa kuvuka 'kigingi' hicho mechi zao mbili zilizosalia hazitakuwa ngumu, pia inacheza kwa kuangalia matokeo ya Yanga," alisema Mayay.
Joseph Kanakamfumu alisisitiza ubingwa wa Simba upo wazi, lakini wakitulia na wachezaji kupewa tiba ya saikolojia anaamini wamevurugwa na kilichotokea baada ya kupewa pointi na kamati ya saa 72 na kisha kupokwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya wachezaji juzi.
Simba imebaki na michezo mitatu  kama itashinda yote itafikisha pointi 68 huku Yanga yenye michezo mitano kama itashinda yote itafikisha pointi 71, ingawa timu zote pia zimetinga nusu fainali ya Kombe la FA.

       comment, like and share
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: