Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli
Rais wa Tanzania John Magufuli amemfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo.
Taarifa kutoka ikulu imesema uamuzi huo wa Rais umeanza kutekelezwa mara moja, na kuwa nafasi hiyo itajazwa baadaye.
Dkt Magufuli amechukua hatua hiyo saa chache baada ya kumshauri Prof Muhongo ajiuzulu.
Rais alitoa wito huo alipokuwa anapokea taarifa ya kamati maalum aliyoiunda kuchunguza mchanga wa madini uliokuwa katika makontena zaidi ya 200 aliyoyazuia yasisafirishwe, kwa ajili ya uchunguzi.
Ripoti iliyowasililishwa katika ikulu ya Tanzania, iliwasilishwa na kamati ya wataalam wa sekta ya madini kubaini aina na kiwango cha madini yaliyo ndani ya mchanga unaosafirishwa kwenda nje.
Katika makontena zaidi ya 200 yaliyokuwa yakichunguzwa, imebainika kuwa yalikuwa na dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni moja za Tanzania.
Dkt Magufuli alivunja Bodi ya wakala wa ukaguzi wa madini Tanzania TMAA na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.
Imebainika kwamba Prof Muhongo alikuwa ameufuata ushauri wa Dkt Magufuli na kuomba kuachishwa majukumu.
Alikuwa amemwandikia barua rais Magufuli kumfahamisha kwamba amejiuzulu.
"Mheshimiwa Rais, napenda kukufahamisha kwamba nimejitahidi kufanya kazi kwa uwezo wangu kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini tangu uliponiteua kuwa waziri tarehe 12 Desemba 2015," aliandika.
"Kutokana na ripoti iliyowakilishwa na Kamati yako Teule ya kuchunguza suala la Makinikia na Mapendekezo yaliyowasilishwa kwako kuhusu Mikataba ya Madini, Utendaji wa Wakala wa Madini (TMAA) na Wizara, Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya uwaziri kuanzia leo."
"Nashukuru sana kwa miongozo yako ya kazi ambayo daima imenisaidia sana kwenye utekelezaji wa majukumu yangu."
Prof Muhongo amefutwa kazi takriban miezi miwili baada ya waziri mwingine, Nape Moses Nnauye , aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufutwa kazi.
Dkt. Magufuli alimteua Dkt. Harrison George Mwakyembe kushikilia wadhifa huo.
Bw Nauye alivuliwa majukumu yake siku moja baada yake kupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu uvamizi uliotekelezwa na mtu anayedaiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika studio za kituo cha habari cha kibinafsi cha Clouds siku chache awali.
Kamati hiyo, kwenye ripoti yake, ilionekana kumkosoa Bw Makonda na kusema alitumia vibaya mamlaka yake.
Kamati hiyo ilipendekeza, miongoni mwa mengine, kwamba Bw Nnauye awasilishe malalamiko ya waandishi wa habari dhidi ya mkuu huyo wa mkoa kwa Rais wa Tanzania pamoja na kuanzishwa kwa uchunguzi dhidi ya polisi waliongia na silaha za moto kwenye chombo hicho cha utangazaji.
Akipokea ripoti hiyo, Bw Nnauye pamoja na kuwataka viongozi wa umma kufanya kazi kwa uweledi, aliahidi kukabidhi taarifa hiyo kwa mamlaka za juu zaidi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kutokana na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo.
0 Post a Comment:
Post a Comment