Mgombea wa ubunge jimbo la Kinondoni kupitia Chadema, Salum Mwalimu amelalamikia uchaguzi huo kuwa mawakala wa chama hicho wamezuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura kwa wakati.
Akizungumza leo Februari 17, 2018 amesema mawakala wa chama hicho kikuu cha upinzani wamechelewa katika baadhi ya vituo kwa saa mbili hadi tatu.
Mwalimu alitolea mfano Kata ya Hananasifu kuwa mawakala hao wameingia saa 2 asubuhi wakati vituo vyote 613 vya kupigia kura vimefunguliwa saa 1 asubuhi.
Mwalimu ambaye alitembelea kituo cha Hananasifu B, amesema mawakala hawa wamezuiwa baada ya kuelezwa kwamba hawana fomu za halmashauri na wengine zile za kiapo.
"Cha ajabu nimeingia kituo kimojawapo halafu wakala wa chama cha UMD anazo barua zote tangu saa 12 asubuhi wakati huohuo wakala wa Chadema hana barua na nilipohoji wananiambia mbona wakala wa CCM pia hana barua na hajaingia,” amesema Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar,
"Sasa mtu anapoanza kukuuliza mbona na wa CCM hana unaanza kujiuliza maswali mengi kwanini? Mle ndani walivyokaa wamejipanga kufanya wanachokifanya na wao wanajua wanafanya kazi kwa maelekezo ya nani.”
Amedai tatizo kama hilo pia limewahi kujitokeza kata ya Saranga na kusababisha upigaji kura kutozingatia haki na taratibu.
Mwalimu amesema baadhi ya wananchi wameshindwa kupiga kura kutokana na majina yao kutoonekana vituoni wakati katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, walipiga kura katika vituo hivyo hivyo.
Mwenyekiti NEC atembelea vituo
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage ametembelea kituo cha kupigia kura cha Leaders Club kuangalia upigaji kura unavyoendelea.
Amesema vituo vimefunguliwa kwa wakati na wapigakura wanaendelea kupiga kura katika kata nane na majimbo mawili yenye marudio ya uchaguzi.
Kuhusu malalamiko kwenye baadhi ya vituo vya kupiga kura amesema hadi sasa hajapokea malalamiko hayo na kwamba mawakala na wasimamizi wa uchaguzi wanashirikiana vyema.
"Hadi sasa nimepokea malalamiko ya wakala mmoja kuwa na viapo viwili. Wakala anayemwakilisha mgombea mmoja hawezi kuwa na viapo viwili,” amesema Jaji Kaijage.
Alipoulizwa kuhusu viapo kucheleweshewa kwa mawakala wa vyama vya siasa amesema wakala anatakiwa kuwa na kiapo kabla ya muda wa uchaguzi kuanza ambapo wakala atatakiwa kuwa na barua ya utambulisho pamoja na kitambulisho.
0 Post a Comment:
Post a Comment