Maafisa wawili nchini Burundi wamefungwa gerezani baada ya rais wa nchi hiyo kuchezewa rafu kwenye mechi waliyoiandaa.
Rais Pierre Nkurunziza ni mlokole kutoka kanisa la Evangelical Christian ambaye mara nyingi hutumia muda wake kusafiri nchini Burundi akiwa na timu yake, Haleluya FC.
Husafiri na kwaya yake yenye jina la Kirundi ''Komeza Gusenga'' ikimaanisha 'omba bila kukoma'
Timu yake hivi karibuni ilipambana na timu ya Kiremba, kaskazini mwa Burundi
Kwa kawaida wachezaji wa timu upinzani hufahamu kuwa wanacheza dhidi ya Rais wa nchi hiyo, na imeelezwa kuwa mara nyingi wachezaji hucheza kwa nidhamu na umakinifu mkubwa kwenye mchezo, hata wakati mwingine kumuachia Nkurunziza afunge bao wakati wa mechi.
Lakini timu ya Kiremba ilikuwa na wachezaji ambao baadhi yao walikuwa wakimbizi kutoka Congo, hawakujua kuwa walikuwa wanacheza dhidi ya rais wa Burundi.
Walishambulia vikali kila wakati aalipouchukua mpira na mpira na kumfanya aanguke mara kadhaa, mmoja wa walioshuhudia ameliambia shirika la habari la AFP kutoka Ufaransa.
Maafisa wa timu ya Kiremba Cyriaque Nkezabahizi na msaidizi wake, Michel Mutama, walifungwa gerezani siku ya Alhamisi, shirika hilo limeeleza.
Mechi hiyo ilichezwa mnamo 3 Februari.
AFP imenukuu vyanzo vya mahakama vikisema walikamatwa kwa makosa ya ''kula njama dhidi ya rais''.
Rais Nkurunziza na serikali yake walinyooshewa kidole na ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka 2017 ikisema kuna ushahidi wenye uzito kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu unaotendeka nchini Burundi.
Ripoti zilisema vikosi vya serikali, lakini pia makundi ya upinzani, vilitekeleza vitendo vya mauaji, kutesa watu na ubakaji baada ya kuibuka kwa machafuko mwaka 2015.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu.
0 Post a Comment:
Post a Comment