Mambo sita yaliyotikisa wiki ya kwanza ya Bunge la Bajeti

  • Wakati hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha 2018/19 ikiendelea kujadiliwa bungeni, mambo sita yametikisa katika mjadala huo, ikiwamo matukio ya mauaji na utekaji.
Mengine yaliyotikisa wiki hiyo ya kwanza ya Bunge ni kuondolewa kazini kwa watumishi wenye elimu ya darasa la saba na msajili wa vyama vya siasa kupewa rungu la kuvifuta vyama vinatakavyokiuka kanuni na sheria.
Suala lingine ni utekelezaji wa operesheni ya uvuvi haramu nchini, demokrasia na uamuzi wa kambi ya rasmi ya upinzani kutosoma bajeti mbadala bungeni.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) Hussein Bashe, akichangia hotuba hiyo iliyosomwa bungeni Jumatano iliyopita na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema yapo mambo yanayoanza kutokea nchini yanayoashiria kuwapo kwa migawanyiko katika Taifa.
“Mambo haya tukiendelea kuyatizama, hayaleti taswira njema huko mbele na wala hayatalifanya Taifa hili kuwa moja wala kupambana na adui mkubwa ambaye ni umaskini,” alisema.
Bashe alisema matukio mengi yanayotokea yanakosa majibu akitoa mfano wa tukio la kijana Allan Mapunda aliyefariki dunia hivi karibuni mkoani Mbeya ikidaiwa kuwa sababu ni kipigo.
“Naiomba Serikali kwa heshima kabisa, matukio ya namna hii yakiendelea kujengeka katika nchi yetu, na ku -develop culture ya impunity (kujengeka kwa utamaduni wa kutowajibika) yanaharibu amani iliyo katika Taifa,” alisema.
Akizungumzia suala kama hilo katika mwongozo alioomba juzi asubuhi bungeni, Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alisema Machi 25 mjini Mtwara, kijana anayeitwa Abdillahi Abdulrahaman alipigwa risasi na polisi akiwa anaokota kungwa baharini ili aweze kufanya kitoweo.
“Nilikuwa naomba kauli ya Serikali kwa sababu bado sijapata kauli ya kuhusu tukio hili. Serikali inatoa kauli gani juu ya kufanya uchunguzi wa kijana huyu pale Mtwara mjini,”alisema.
Hotuba za upinzani kutosomwa
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe alisema hawatasoma hotuba yoyote mbadala hadi hapo watumishi wa sektarieti yake waliofukuzwa Januari mwaka huu watakaporejeshwa.
Kauli hiyo ya Mbowe, ilikuja baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutamka bungeni kuwa hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu haitawasilishwa bungeni kwa sababu ya kuchelewa kuwasilishwa katika Ofisi za Katibu wa Bunge.
Mbowe alisema kutowasilishwa kwa hotuba hiyo kulitokana na kukosekana kwa watumishi hao ambao shughuli zao ni kuchambua, kutafiti na kuandika hotuba za kambi hiyo.
“Baada ya kikao chetu, tumekubaliana kuwa hakutakuwepo na hutuba za upinzani bungeni hadi pale watumishi hao watakaporejeshwa kufanya shughuli hizo,” alisema.
Ukuaji wa demokrasia
Akichangia hotuba ya bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Pareso alisema tangu Awamu ya Tano iingie madarakani, imeonyesha jitihada za kuua vyama vya upinzani kwa kuvinyima haki yake ya kimsingi.
“Utaendeleaje kupima kuwa vyama vya siasa vinafanya kazi kama hakuna mikutano ya hadhara? Vyama vya siasa ni kama makanisa leo mtu anajiunga kesho anatoka,” alisema.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisema miaka 26 tangu mfumo wa vyama vingi uanze nchini, uhuru wa kujiunga na vyama vya siasa kwa kuridhishwa na itikadi zake umeongezeka.
Kufutwa kwa vyama vya siasa
Licha ya Waziri Mkuu kusema katika hotuba yake kwamba msajili wa vyama vya siasa anasimamia vyema suala la demokrasia, Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Salim Hussein alisema hakubaliani na hilo.
Alisema msajili wa vyama vya siasa badala ya kusimamia ili viende mbele, amekuwa anavikandimiza na pia amepandikiza mgogoro CUF.
“Msajili huyo kamwandikia barua (mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili, Profesa Ibrahim) Lipumba kwamba hatatoa ruzuku kwa sababu chama kina mgogoro pia akamwandikia katibu mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) barua hiyohiyo lakini amempa Lipumba Sh1.3.”
Operesheni uvuvi haramu
Wabunge wa CCM wanaotoka maeneo yenye wavuvi, walilalamikia operesheni ya uvuvi haramu inavyoendeshwa. Wabunge hao, Dk Raphael Chegeni (Busega), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Joseph Musukuma (Geita Vijiji), Aeshi Hillary (Sumbawanga Mjini) na Costatino Kanyasu (Geita Mjini), walisema wavuvi wengi wana vipato duni na kuchomwa kwa nyavu zao kunasababisha ukosefu wa ajira.
Timua ya watumishi
Musukuma pia aliibua hoja ya watumishi wa darasa la saba kuondolewa kazini na kutaka warudishwe kwani wana mchango mkubwa kwa Taifa, “Sasa huku ndani (bungeni) kuna darasa la saba wengi na hata mliokuwa na elimu ya juu mna watu ambao wanafanya kazi ndogondogo darasa la saba. Ninashangaa kwa nini wamewafukuza watendaji wa kijiji wa darasa la saba?” alihoji.
Suala hilo lililungwa mkono na Kanyasu, Profesa Tibaijuka na Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu.
Wachambuzi
Akitoa maoni yake kuhusu mijadala hiyo, Profesa Haji Semboja wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema, “Bunge ni chombo kinachowakilisha uhalisia wa maisha ya wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lakini mifumo ya demokrasia imefungwa huku nje ya Bunge, makanisa yakizungumza yanashambuliwa, waliokuwa wanazungumza ukweli sasa wamefyata mkia.”
Alisema anaamini kwa usikivu wa Rais John Magufuli, ambaye amekuwa ni mpigania wanyonge, atasikiliza hoja hizo.
Wakili wa kujitegemea, Onesmo Kyaruki alisema baadhi ya hoja hizo zina mashiko na zinatakiwa kufanyiwa kazi na Serikali.
Alisema hoja ya darasa la saba kwa watumishi inahitaji kuangaliwa upya kutokana na mchango walioutoa katika sekta mbalimbali nchini.
“Tumefundishwa na walimu wa Upe, kama mtumishi ametumika miaka mingi, halafu unamfukuza miaka mitatu kabla ya kustaafu inashangaza, kama ni kuwaondoa, basi tuwe na utaratibu maalumu,” alisema.

Download App YETU hapa⬇⬇



Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: