Utata waibuka mapambano ya polisi, wananchi Kibiti



Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Onesmo
  
 Hali ya maisha kwa wakazi wa Jaribu wilayani Kibiti imeendelea kuwa ya hofu, baada ya jana polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi, huku mmoja akijeruhiwa.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema lilitokea jana mchana baada ya wananchi wa eneo hilo kukaidi amri iliyotolewa na Jeshi la Polisi.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya askari wanane kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana walioshambulia gari la Jeshi la Polisi Aprili 13 katika Kijiji cha Jaribu Mpakani. Tangu wakati huo kumekuwa na msako na ulinzi mkali katika eneo hilo.
Mkazi wa kijiji cha Jaribu Mpakani aliyeshuhudia tukio la jana na ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema walikimbia baada ya kuwaona polisi kwa kuwa wamekuwa wakiwapiga.
Habari zilizopatikana zilisema mwananchi ambaye hajatambulika jina amelazwa hospitali baada ya kupigwa risasi na askari polisi wanaoendesha operesheni ya kuwasaka watu ambao wamekuwa wakifanya uhalifu katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga hakukana wala kuthibitisha tukio hilo alipoulizwa na Mwananchi jana, badala yake akasema wanafuatilia.
Emmanuel Humbi, ambaye ni daktari wa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi, alisema jana walimpokea majeruhi aliyepigwa risasi chini ya kwapa la kushoto.
Alisema risasi hiyo imeharibu pafu na kuvunja mbavu mbili.
Alisema mipango ilikuwa ikifanyika ili kumhamishia majeruhi huyo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hata hivyo kumekuwa na taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa kuhusu hali ilivyokuwa jana, baadhi wakisema mbali na kujeruhi, kulikuwa na mtu aliyefariki katika tukio hilo.
Taarifa zisizo rasmi zinasema mtu aliyejeruhiwa alikataa kutii amri ya polisi ya kumtaka asimame na alipojaribu kukimbia alipigwa risasi na polisi.
Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani alisema jeshi hilo litatoa taarifa rasmi kama ni kweli polisi wamewaua watu katika tukio hilo.
“Sisi hatufanyi kazi kwa tetesi. Kama kuna habari kama hizo, tutazitoa katika mkutano na waandishi wa habari na si kuzungumzia tetesi,” alisema.
Wilaya hizo za mkoani Pwani zimekuwa zikikumbwa na matukio ya viongozi wa vijiji, watendaji na askari kuuawa.
Katika tukio la hivi karibuni, polisi nane waliokuwa wakitoka zamu walishambuliwa kwa risasi na watu waliokuwa wamejificha kando ya barabara.
Matukio ya Mauaji Pwani
Mei, 2016: Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Saidi Mbwana aliuawa kwa kupigwa risasi.
Oktoba 2016: Aliyekuwa ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ally Milandu aliuawa baada ya kuvamiwa na watu wanne, waliompiga risasi mbili.
Novemba, 2016: Wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho waliuawa kwa kupigwa risasi.
Januari 19, 2017: Katika kijiji cha Nyambunda, kitongoji cha Mkwandara, watu wasiofahamika walimuua mfanyabiashara, Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.
Februari 2017: Watu wasiofahamika walivamia nyumba ya mwenyekiti wa kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga, ambaye alifanikiwa kuwatoroka. Hata hivyo majambazi hayo yalipomkosa, yalirejea na kumwaga mafuta, kisha kuichoma moto nyumba yake.
Februari 24: Watu wasiofahamika walimuua ofisa upelelezi, Peter Kubezya na maofisa maliasili wawili.
Machi 2017: Polisi iliwaua kwa kuwapiga risasi watu watatu waliovalia kike wakati walipojaribu kukwepa vizuizi vitatu vya barabarani wakiwa na pikipiki mbili. Waliuawa katika daraja la Mkapa.
Aprili 13: Polisi wanane waliuawa na watu wasiofahamika katika kijiji cha Jaribu Mpakani wilayani Kibiti.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga hakukana wala kuthibitisha tukio hilo alipoulizwa na Mwananchi jana, badala yake akasema wanafuatilia. 
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: