Mwalimu wa shule ya msingi amuua mwanaye kwa kipigo

 


 Polisi mkoani Mwanza inamshikilia mwalimu wa Shule ya Msingi Mwamakoye wilayani Kwimba kwa tuhuma za kumchapa mtoto wake na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea Aprili 21 mwaka huu, saa kumi jioni na kumtaja marehemu kuwa ni Sifael Emmanuel (8) mwanafunzi wa shule hiyo.
Msangi alisema taarifa zilizopatikana zinasema kuwa, mtoto huyo alikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani pindi anapoagizwa dukani na mama yake.
“Kutokana na tabia hiyo mama yake alikuwa akimpatia adhabu, lakini hakukoma na kwamba juzi mtoto huyo aliagizwa tena dukani na kuendelea na tabia yake ileile,” alisema.
Kamanda alieleza zaidi kuwa mtoto huyo aliporejea kutoka dukani, baba yake alimshika na kuanza kumshushia kipigo kwa muda mrefu.
“Wakati anaendelea kumpiga, mtoto alikuwa akilia na akaishiwa nguvu na baada ya muda mfupi akapoteza maisha,” alisema Msangi
Kutokana na tukio hilo, wananchi walioshuhudia walitoa taarifa kituo cha polisi na baadaye mwalimu huyo alikamatwa na kupelekwa kituoni.
Aliongeza kuwa kwa sasa baba wa mtoto huyo anahojiwa na polisi hadi uchunguzi utakapokamilika na atafikishwa mahakamani.
Pia, Msangi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa ajili ya uchunguzi na kwamba, utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Kamanda huyo aliwaonya baadhi ya wazazi wanaowafundisha watoto wao kwa kuwachapa na fimbo huku akiwataka kutumia namna nyingine ya kuwaelekeza wanao.
Vilevile, alishauri kuwa ni vyema zaidi kuwaonya watoto kwa maneno ya hekima au vitabu vya dini ili kuepuka adhabu zinazoweza kuleta madhara.
Akizungumzia tabia ya baadhi ya wazazi kuwaadhibu watoto wao kwa kuwachapa fimbo, mkazi wa Nyamanoro, Amina Lusheshu alisema ni vyema adhabu ikatolewa kwa kuzingatia umri.

Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: