Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ameitisha kurejelewa kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani nchini humo.
Kadhalika, amesema kwamba anataka uchaguzi wa majimbo ufanyike.
Amesema hayo baada ya maandamano mengine makubwa kupangwa na upinzani Jumatatu, wiki tatu baada ya maandamano mengine makubwa kutatiza shughuli nchini humo.
Waandamanaji wamekuwa wakitaka uchaguzi mkuu ambao umepangiwa kufanyika mwaka ujao ufanyike mwaka huu na Rais Maduro aachie madaraka.
Mazungumo kati ya upinzani na serikali mwaka jana yalivurugika baada ya upinzani kumtuhumu Bw Maduro kwa kukiuka baadhi ya makubaliano na kutumia mazungumzo hayo kujipatia muda zaidi wa kuendelea kuongoza.
Akihutubu kupitia runinga Jumapili, bw Maduro aliunga mkono pendekezo la kufanyika kwa ucahguzi wa mameya na magavana wa majimbo lakini hakugusia uchaguzi wa urais.
"Uchaguzi - ndio, Ninataka uchaguzi sasa," alisema.
"Hili ndilo ninalosema kama kiongozi wa nchi, kama kiongozi wa serikali."
Uchaguzi wa magavana wa majimbo ulifaa kufanyika Desemba mwaka jana, lakini uchaguzi wa mameya ulifaa kufanyika mwaka huu.
Maandamano makubwa ya upinzani yalifanyika Jumamosi, waandamanaji wakiwa kimya kwa heshima ya watu 20 waliouawa katika maandamano ya karibuni.
Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wanasema watu zaidi ya 1,000 walikamatwa wakati wa maandamano hayo na 700 bado wanazuiliwa.
Upinzani unailaumu serikali kwa mgogoro wa kiuchumi ambao umeathiri pakubwa nchi hiyo na kusababisha uhaba wa vyakula, bidhaa muhimu na dawa.
Maandamano yalichocheza na jaribio la Mahakama ya Juu inayodhibitiwa na serikali kutwaa baadhi ya mamlaka ambayo huwa na Bunge.
0 Post a Comment:
Post a Comment