Wanafunzi watatu kutoka shule ya msingi ya Butwa mkoani Geita wamekufa maji huku wenzao tisa wakinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka katika Ziwa Victoria.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo amesema tukio hilo lilitokea Jumatatu jioni wakati wanafunzi hao wakitoka shuleni kuelekea nyumbani kitongoji cha Lulegeya
Amesema wanafunzi hao ambao wote ni wasichana wana umri kati ya miaka 9 hadi 13. Miili yote imepatikana na kukabidhiwa kwa familia zao
Akielezea tukio lilivyotokea, Kamanda Mwabulambo anasema wakiwa katikati ya maji, nahodha wa mtumbwi huo uliokuwa umebeba wanafunzi 12 alihofia idadi ya abiria kuwa ni kubwa na hivyo kuamua kurudi nchi kavu ili apunguze abiria hao.
Lakini kabla ya kufika nchi kavu, baadhi ya wanafunzi walihamia upande mmoja wa mtumbwi na kusababisha uzito kuzidi na ndipo mtumbwi huo ulipopinduka umbali wa mita 20 kutoka nchi kavu.
Wanafunzi tisa wa kiume walifanikiwa kuogelea hadi kufika nchi kavu na kuokoa maisha yao.
Kamanda Mwabulambo amesema polisi inamshikilia mmiliki wa mtumbwi huo uliopinduka kwa mahojiano zaidi kujua undani wa ajali hiyo.
Mtumbwi ndio njia kuu ya usafiri katika visiwa vilivyopo Ziwa Victoria lakini mingi ipo katika hali mbaya na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara.
0 Post a Comment:
Post a Comment