MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Richard Kwitega kuwarudisha watendaji watatu wanaotuhumiwa kusababisha upotevu wa fedha kiasi cha Sh milioni 246.4 katika sekta ya afya na nyingine.
Gambo aliyasema hayo jana wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake, ambayo alikutana na watumishi wa Jiji la Arusha, viongozi wa dini, wananchi pamoja na vikundi vya kinamama vinavyopewa mkopo bila riba wa Sh milioni 100 kwa kinamama 500 wajasiriamali wadogo. Aliwataja watumishi hao wanaotakiwa kuitwa kuwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Juma Idd ambaye katika uteuzi wa Rais John Magufuli aliachwa, Mweka Hazina wa Jiji, Kessy Mpakata aliyehamishiwa mkoa wa Shinyanga na Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Bakari Salumu ambaye amehamishiwa Tamisemi, Dodoma.
Mwingine ambaye anakabiliwa na tuhuma hizo lakini bado yuko kwenye utumishi hapa Arusha ni Katibu wa Afya, Optat Ismail. Mkuu wa mkoa alisema watu hao wanaostahili kuandikiwa barua kwenda kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili aliyekuwa mkurugenzi huyo Idd na wenzake warudi kwenye vituo vyao vya kazi vya awali ili kujibu tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika sekta mbalimbali.
Alisema watu hao warudishwe Jiji la Arusha ili kujibu tuhuma hizo na ikithibitika kama hawajahusika na tuhuma zinazowakabili, wataendelea na majukumu yao ya kila siku. “Watu hawa ni lazima warudishwe Jiji la Arusha ili kujibu tuhuma zinazowakabili za upotevu wa fedha mbalimbali ikiwemo fedha za afya kwani wananchi hawapati huduma za afya na nyingine huku baadhi ya watu wakinufaika na fedha za umma.
“Hawa watu wanapaswa kurudi kazini kuja kuonesha kama fedha hizo zimeliwa au zimetumikaje. Haiwezekani fedha zitolewe halafu tume niliyoiunda mimi izungushwe na kujibiwa ovyo kisha Katibu anabembelezwa halafu hatoi ushirikiano, hii ina maana gani nataka wahojiwe hawa watu waeleze fedha hizi ziko wapi,” alihoji Gambo. Pia amempa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia saa 24 kuhakikisha watumishi zaidi ya tisa wanaodaiwa kula fedha za afya zaidi ya Sh milioni 85 kupitia mafunzo hewa wanachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja kuzirudisha fedha hizo.
Alisema inashangaza kuona wananchi wakikosa huduma bora za afya huku wengine wananufaika na fedha za wananchi ikiwemo kununua dawa sehemu zisizostahili. Alisema pia wapo watumishi wanaotumia vibaya fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya kwa madai kuwa zinatumika vibaya na baadhi ya watumishi kwa kujiandikia posho au vikao hewa kwa fedha ambazo hazijalengwa kuingizwa huko.
0 Post a Comment:
Post a Comment