Chama cha upinzani nchini Kenya ODM kimeanza uteuzi wa wagombea wake watakaokiwakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.
Tayari baadhi ya uchaguzi wa chama hicho umekumbwa na utata huku bodi ya kitaifa ya uchaguzi ya ODM, NEB ikifutilia mbali matokeo ya utezi wa gavana wa kaunti ya Busia ilopo katika maeneo ya magharibi mwa taifa hilo, saa chache tu baada ya gavana Sospeter Ojaamong kutangazwa mshindi.
Matokeo hayo yalipingwa na mpinzani wake mkuu Paul Otuoma ambaye ni mbunge wa Funyula katika kaunti hiyo ya Busia.
Katika taarifa, mwenyekiti wa NEB alisema bodi hiyo imegundua kuna hitilafu katika matokeo na "kuyatangaza kama yalivyo kunaweza kusababisha vurugu kati ya wanachama katika kaunti hiyo."
"Kwa mujibu wa sababu hizo, bodi imeamua kufutilia mbali matokeo ya uteuzi wa gavana wa Busia na kuamuru zoezi hilo kurudiwa Jumanne tarehe 25 April, "ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo matokeo ya viti vingine yatasalia kama ilivyopokewa na bodi, Bi Pareno alisema.
Bodi hiyo vilevile imepokea matokeo kutoka kaunti za Machakos na Bungoma ambazo pia zilifanya uteuzi wao siku ya Alhamisi.
Awali, baada ya Ojaamong kutangazwa mshindi wa kiti hicho cha atakayewania ugavana kupitia tikiti ya ODM, wafuasi wa Dkt. Otuoma walifanya maandamano wakipinga matokeo hayo.
Ojaamong alikataa kusema lolote kuhusu uamuzi huo wa bodi.
"Siwezi kulijadili swala hilo kwa sababu sijapata mawasiliano rasmi kutoka kwa bodi.
"Hilo linaweza kutendeka vipi ilhali malalamishi hayajafikishwa kwao rasmi? matokeo yametangazwa muda mchache tu uliopita," alisema.
Ojaamong na Dkt Otuoma wanadaiwa kuelekea Nairobi kukutana na viongozi wa ODM kuhusu swala hilo.
0 Post a Comment:
Post a Comment