MAONI: Matukio ya utekaji yanaathiri taswira ya nchi




 Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilianza kujinadi kwa sera ya uchumi wa viwanda. Lengo ni kuhakikisha kufikia 2020 taifa linakuwa na uchumi wa kipato cha kati. Mahubiri haya yanaendelea kutolewa kuanzia kwa watendaji wa idara, taaisisi, mawaziri mpaka kwa Rais John Magufuli ambaye ni mwasisi wa sera hiyo.
Awali, suala hili liliwavutia watu wengi na kuona kuwa Serikali ya awamu ya tano imeamua kutekeleza mikakati yenye lengo la kumkwamua mwananchi wa hali ya chini. Usiniulize kama sera hiyo inatekelezeka au la.
Hata hivyo, wakati Serikali ikihubiri suala la uchumi wa kati unaotegemea sekta ya viwanda, kuna mambo yanayojitokea hapa nchini yanayoharibu taswira ya Serikali ambayo kwa mujibu wa Katiba, imepewa haki ya kusimamia ustawi wa wananchi na kuwalinda. Nayo ni matukio ya utekaji ambayo yamebadili hadithi tunazosimuliwa kutoka uchumi wa viwanda na kuwa taifa la sinema kila kukicha.
Matukio ya utekaji nchini hayajaanza jana wala juzi. Mwaka 2012 aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka, alitekwa wakati chama chake kikiwa na mgogoro na Serikali kuhusu masilahi ya madaktari nchini. Ulimboka alipigwa, kung’olewa meno na kucha bila ganzi na kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji akiwa hoi. Ulimboka alitekwa wakati chama alichokuwa anakiongoza kikiwa kwenye majadiliano na Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara yao. Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilikana kuhusika na utekaji wa Dk Ulimboka.
Mwaka 2013, mwandishi wa habari mkongwe, Absalom Kibanda naye alikutana na mkono wa watekaji, akiwa njiani kurejea nyumbani kwake. Kibanda alitekwa na watu wasiojulikana na kunyofolewa jicho lake. Serikali haikukamata mtu yoyote aliyehusika.
Hadi sasa, mwanasiasa kijana wa Chadema, Ben Saanane ametoweka na watu wasiojulikana. Kabla ya kutekwa Saanane alijipambanua kupitia mitandao ya kijamii kwa kutoa hoja zilizoibua msisimko miongoni mwa vijana. Alipotea Novemba 2016 na hadi sasa kuna sintofahamu ya ni wapi hasa alipo.
Kelele kuhusu Ben Saanane, zimekuwa mjadala mkuu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kwanini atekwe? Watekaji ni nani? Wana shabaha ipi? Wanataka kutuma ujumbe gani kwa Watanzania?
Chama chake kinalaumu dola na kusema kama inamshikilia ieleze inamshikiria kwa kosa lipi ili apelekwe mahakamani lakini polisi iliyopaswa kuchunguza na kufanya upelelezi hadi sasa haijawaambia Watanzania kuwa Saanane yuko wapi au uchunguzi umefikia wapi.
Kama nilivyosema awali, Serikali kupitia vyombo vyake ndiyo iliyopewa jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao kwa mujibu wa Katiba. Ikiwa mtu anatekwa miezi mitano bila maelezo ya kueleweka kutolewa na vyombo vya usalama wananchi hawana namna zaidi ya kuamini kuwamba vyombo hivyo vimeshindwa kuwalinda.
Kabla vumbi la Saanane halijatua, wiki iliyopita, msanii maarufu nchini Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki naye alitekwa na watu wasiojulikana akiwa ofisini kwake na kupelekwa kusikojulikana na kupatikana Jumamosi akiwa katika Kituo cha Polisi cha Oyster Bay. Kabla ya kutekwa Roma amejitambulisha katika jamii kwa nyimbo za kukosoa ukiwamo ‘Viva Roma’.
Matukio haya hayawezi kutuacha salama kama taifa zaidi ya kuzidi kutuchafua. Matukio haya ni kipimo kwa Serikali kama iko tayari kulinda maisha na ustawi wa taifa. Tanzania si kisiwa, matukio haya ya kifedhuli yanalivua nguo taifa katika jumuiya ya kimataifa.






                             BY Frederick Nwaka  mwandishi wa Mwananchi.     
  
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: