16 Oktoba 2017
Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto wametoa onyo kali kwa mataifa ya nje wakiyashutumu kwa kujaribu kuingilia mambo ya ndani ya Kenya.
Wakizungumza wakati wa mikutano ya kampeni za kisiasa wakiwa Nyahururu na Karatina, viongozi hao walisema nchi haikuwa katika mgogoro wowote hata kustahili kuingiliwa kati na mataifa ya kigeni.
“Nataka kuiambia Jumuia ya kimataifa kwamba Kenya hakuna tatizo. Tatizo pekee tulilonalo ni mtu mmoja anayeitwa Raila Odinga (kiongozi wa Nasa),” alisema Rais Kenyatta.
Mkuu huyo wa nchi alisema nchi yake haitaruhusu mazungumzo kati yake na Odinga yatakayoongozwa na mataifa ya kigeni.
Huku akisisitiza kuwa Kenya ni nchi huru alisema: “Hatutaruhusu wazungu kuja na kutuambia nini cha kufanya. Kama watakuja Kenya, waacheni waje kama watalii. Waacheni waende Wamasai Mara, waje Laikipia na maeneo mengine, lakini wasije hapa na kutuambia nini cha kufanya,” alisema Rais Kenyatta.
Pia alimlaumu Odinga kwa maandamano na uharibifu wa mali katika maeneo mbalimbai ya nchi, akisema mtu yeyote aliyeshiriki katika maandamano lazima ashughulikiwe ipasavyo. Rais aliwaomba wapigakura nchini kujitokeza kwa idadi kubwa ili kupigakura zao kwenye uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
Aidha, Makamu wa Rauis Ruto alimshutumu Odinga kwa kuiomba Jumuia ya Kimataifa kulazimisha mazungumzo ya upatanishi kwa lengo la kuunda Serikali ya Muungano.
“Analialia mbele ya mataifa ya kigeni ili yamuonee huruma na iundwe timu ya kusimamia upatanishi. Lakini hata kama atakwenda Ulaya, Washington apite hadi Mexico au arudi Casablanca, haitakuwepo Serikali ya Nusu Mkate,” alisema Ruto.
Ruto amemtaka Odinga kusitisha maandamano, kuacha uchokozi na vitisho dhidi ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tume Ezra Chiloba na akamtaka ajiandae kwa uchaguzi.
“Kama Jubilee tungetaka kumwapisha Kenyatta kuwa Rais, tungekwisha fanya hivyo, lakini kamwe hatukutaka kuingiza nchi katika machafuko kwa sababu sisi ni wapenda amani. Hivyo tuliamua kurudi kupigakura. Hivyo naye pia asitishe maandamano, aache maonyesho na ajiandae kwa uchaguzi,” alisema Ruto
Akizungumza katika mkutano wa kampeni Karatina, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa suala la kugawana madaraka na wapinzani halipo.
Pia aliwatetea polisi kutokana na madai ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakiandamana dhidi ya IEBC.
Katiba inaruhusu maandamano yenye amani, lakini huwezi kuita maandamano ya amani wakati unawatuma watu wako kurushia mawe vituo vya polisi. Unatarajia kupata nini pale unapokirushia mawe kituo cha polisi?”alihoji rais.
TUFUATE FACEBOOK: zakacheka.blogspot.com na u-download APP ya ZAKACHEKA huko
0 Post a Comment:
Post a Comment