Jengo la abiria kiwanja cha ndege Dodoma kuboreshwa

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, ametoa miezi miwili kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha linakamilisha uboreshaji wa jengo la abiria lililopo katika kiwanja cha ndege cha Dodoma ili kuwezesha jengo hilo kuhudumia abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Ametoa agizo hilo, mkoani Dodoma katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uboreshaji wa jengo baina na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) na NHC na kusema  kuwa kukamilika kwake kutawezesha abiria zaidi ya 100 kuhudumiwa kwa wakati mmoja ambapo kwa sasa jengo linahudumia abiria 35.

“Mkataba tunaoshuhudia ukisainiwa leo unaitaka NHC kukamilisha mradi huu ndani ya miezi mitatu lakini niagize mradi huu ukamilike ndani ya miezi miwili kwa sababu fedha zipo na cheti mlichonacho cha daraja la kwanza kinaonyesha namna mnavyoweza kufanya kazi hii kwa haraka’ alisema Mhandisi Nditiye.

Aidha Naibu Waziri Mhandisi Nditiye ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), pamoja na maboresho hayo kuhakikisha inafanya maboresho kwa kujenga maduka ya kubadilishia fedha na bidhaa ili abiria watakaotumia kiwanja hicho hiyo waweze kupata huduma mbalimbali wakati wanaposubiria kupanda ndege.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa ndio Makao Makuu ya Serikali hivyo miradi yote inayotekelezwa chini ya Wizara lazima izingatie viwango na thamani ya fedha ili kuendana na hadhi ya mji.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Mheshimiwa Antony Mavunde ameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo na kumuomba Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, kuwafikiria wananchi waliopisha upanuzi wa kiwanja hicho kwa kuwalipa fidia mapema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali hapa nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga.

Ameongeza kuwa Serikali imepanga kujenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa katika eneo Msalato ambapo kwa sasa wataaalam wanapitia usanifu wa kiwanja hicho na wakati wowote zabuni itatangazwa ambapo kiwanja hicho kitaweza kuhudumia ndege kubwa za kisasa kwani kinatarajiwa kuwa barabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa Kilomita 4.5 mpaka 5.

Awali akitoa taarifa yake kabla ya utiaji saini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Richard Mayongela, amesema kuwa Fedha zinazotumika kukarabati jengo hilo ni fedha za ndani za mamlaka hivyo jengo hilo litakamilika kwa wakati na viwango.

Uboreshaji wa jengo la abiria lililopo katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma utagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 600 na utahusisha mifumo ya kisasa ya Tehama, mifumo na maji taka , mifumo ya matangazi ya ratiba za ndege pamoja na mgahawa.

Download App YETU hapa⬇⬇



Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: