CCM MPYA: wanasiasa wakongwe wanena

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM=>


UAMUZI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kupitisha majina mengi mapya katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chama hicho, yameelezwa kuwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba ndani ya chama.
Wanasiasa wakongwe na wachambuzi waliozungumzia na HabariLeo jana walisema uteuzi wa majina mapya ndani ya CCM, ni mkakati wa CCM wa kufanya mageuzi kwa kuja na watu wenye falsafa na itikadi mpya ndani ya chama.
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa alisema kupitishwa kwa majina mapya mengi haimaanishi kuwa chama kinajisafisha bali ni mwendelezo wa kujitathmini kupitia falsafa yake ya kujivua gamba iliyoasisiwa mwaka 2011.
Msekwa alisema baada ya CCM kufanya vibaya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hasa kutokana na kura za mgombea urais wa CCM wakati huo Jakaya Kikwete kuporomoka, CCM iliamua kufanya tathmini ya kutaka kujua kwa nini wananchi walianza kupoteza imani na chama chao.
Alisema kuwa ndani ya CCM, tathmini siyo jambo jipya bali ni mradi endelevu unaofanyika kila mara kwa lengo la kukiimarisha chama ili kiendelee kuaminika na wananchi na wana CCM wenyewe.
“Tumekuwa tukifanya tathmini kila baada ya uchaguzi, kwa hiyo CCM kuingiza sura mpya katika uongozi ni miongoni mwa mabadiliko muhimu ndani ya Chama. Mabadiliko hayo yanawapa fursa wanachama wengi kushika nafasi za uongozi badala ya watu wachache kuhodhi nafasi hizo, zamani ilikuwa mtu mmoja anashika nafasi nyingi, huyo huyo mbunge na mwenyekiti wa chama,” alieleza Msekwa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine (SAUT), Dk Charles Kitima alisema kuingizwa kwa sura nyingi mpya kwenye safu ya uongozi, ni mkakati wa CCM wa kufanya mageuzi kwa kuja na watu wenye falsafa na itikadi mpya ndani ya chama.
Alisema mageuzi ambayo CCM inayafanya ni kutaka kukirudisha chama kwenye uasili wake. Alisema CCM kina itikadi nzuri, tatizo waliruhusu watu wachache kukiondoa chama mikononi mwa wengi na kukiweka mikononi mwa kikundi kidogo cha watu, hivyo kitendo cha kuleta kizazi kipya cha uongozi, kinaweza kuwa sehemu ya mkakati wao wa kujisafisha.
“CCM iligeuka kuwa chama cha matajiri. Ilikuwa jambo la kawaida kuona watu wakubwa kwenda kugombea nafasi za chini za uongozi kama vile udiwani ili wazitumie nafasi hizo kufanya biashara zao na siyo kuwatumikia wananchi,” alieleza Dk Kitima.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa kuingizwa kwa sura mpya nyingi kwenye nafasi za uongozi ni mpango wa CCM kuzaliwa upya. Alisema Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Magufuli ameona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ili chama kiendane na wakati.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema kuwa mabadiliko ya kuingiza sura mpya kwenye uongozi ndani ya CCM, unaweza kuwa mkakati wa kuwa na CCM mpya kwa kujenga maadili ndani ya chama, lakini pia kukirudisha kwa wanachama wake. “Nyuso mpya ni uhai wa chama.
Viongozi hao watakuja na nguvu, mitazamo na maono mapya ndani ya chama. Viongozi kama ni walewale wakati wote, huwezi kuwa na vitu hivyo,” alisema Profesa Bana. Uchaguzi 2019/2020 Kuhusu mkakati wa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020, Msekwa alisema hana mashaka na timu mpya ya uongozi kwa kuwa chama ni wanachama.
Alisema chama kina Katiba na miongozo ambayo wanachama lazima waifuate. Kwa mujibu wa Msekwa, pamoja na mambo mengine, viongozi hao jukumu lao ni kusimamia katiba na taratibu za chama katika nafasi zao na kuhamasisha wanachama wakati wa uchaguzi ili chama kiendelee kushika dola na kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake, Profesa Bana alisema kuwa utafiti wa Twaweza ulionesha kuwa wananchi wameanza kuwa na imani tena na serikali na CCM kutokana na mageuzi makubwa, yanayofanywa ndani ya serikali na chama.
Alisema kutokana na hali hiyo, kipimo cha kwanza kwa CCM ni katika uchaguzi wa madiwani utakaofanyika keshokutwa katika kata 43, kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.
Kuhusu mikakati hiyo ya uchaguzi, Dk Kitima alisema kuwa ni jambo la msingi kwa chama cha siasa kuwa na watu watakaoleta ushindi ili kiendelee kushika dola. Alisema nguvu ya ushindi wa chama iko kwa wapiga kura, hivyo ni muhimu kuwa na viongozi watakaokuwa wanawatumikia na kuishi pamoja na wananchi.
“Tatizo la vyama vyetu vya siasa havijaja na falsafa ya maendeleo ya nchi na matokeo yake badala ya nchi kusonga mbele kimaendeleo inabaki hapohapo miaka yote, hivyo uongozi mpya uwe na dira nzuri ya maendeleo, mabadiliko ya kweli lazima yaanze na viongozi wenyewe kwa kuja na dira na mwelekeo mpya wa kimaendeleo,”alisema Dk Kitima.
Upinzani kuhamia CCM Aidha kuhusu wimbi la wanasiasa wa upinzani kuhamia CCM, Msekwa alisema sababu zinazowafanya wanasiasa kuhama chama kimoja na kwenda kingine zinafanana, lakini kubwa ni mbili ambazo ni kutoridhishwa na mwenendo wa mambo ndani ya vyama vyao, lakini pia ni kuvutiwa na hali nzuri ya chama anachokwenda.
Msekwa alisema hata ndani ya CCM, kuna wanachama waliohamia upinzani baada ya kutoridhika majina yao kutopitishwa kugombea nafasi za uongozi kwa ngazi ya urais, ubunge na nyinginezo.
Alisema sababu hizo ndizo hasa zinawafanya wanasiasa kuhama vyama vyao. Sababu nyingine kwa mujibu wa Profesa Bana ni kuwa Rais Magufuli amekuwa akijibu kwa vitendo na kwa kasi hoja zote, zilizokuwa zikisemwa na upinzani kama vile mambo ya rushwa, ufisadi na watuhumiwa wa vitendo hivyo kufikishwa mahakamani, ndiyo sababu inayowarudisha wanasiasa hao ndani ya CCM.
Profesa Bana alisema itachukua muda mrefu kwa upinzani nchini, kuaminiwa na wananchi katika uongozi wa nchi kwa kuwa unaonekana kama kupoteza mwelekeo. Alisema upinzani wanatakiwa waje na maono mapya ya kisiasa badala ya kuendelea tu kupinga juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Naye Dk Kitima alisema wanasiasa wanaohama vyama wanaweza kuwa na ndoto na nia nzuri ya kisiasa, lakini baadhi yao wamekuwa na sababu za kimaslahi. Alisema wanaohamia CCM wasifanye hivyo kwa kutafuta fursa bali wawe na nia nzuri ya kuleta maendeleo kwa nchi. Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ilikutana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu, Dar es Salaam juzi chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais John Magufuli.
Aidha, viongozi wengi wenye nyadhifa zaidi ya moja serikalini na CCM hawakupitishwa, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliyekuwa pia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya.
Juzi, NEC ilifanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za wenyekiti wa mikoa, NEC mikoa na Katibu Mwenezi wa mikoa na jumuiya za chama hicho. Katika uteuzi huo, NEC haikuwarudisha viongozi wengi wa mikoa, wajumbe wa NEC na makatibu wa uenezi katika kile kilichoonekana ni kujipanga vyema kwa chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Katika hotuba zake, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Magufuli amekuwa akisema wazi kuwa chini ya utawala wake katika CCM, hataruhusu mtu yeyote kuvaa kofia nyingi ndani ya chama hicho.
Ni kutokana na msimamo huo, vigogo wa CCM mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Katavi na Manyara hawakuwania nafasi hizo. Mkoa wa Dar es Salaam, sura mpya zilizoteuliwa ni pamoja na Dk Malima Bundara, Waziri wa zamani, Kate Kamba na Brigedia Jenerali mstaafu, Ryakitimbo Magige.
Waliopitishwa kuwania nafasi za Katibu wa Siasa na Uenezi mkoa wa Dar es Salaam ni Simon Mwakifamba, Fikiri Mzome, Mashaka Nyadhi na William Mlenge ambao wote ni wapya.
Mkoa wa Dar es Salaam haukufanya vyema katika uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge mwaka 2015, ambapo majimbo ya ubunge ya Kawe, Ubungo, Kibamba, Kinondoni na Temeke yalienda upande wa upinzani.
Kwa Mkoa wa Dodoma, NEC ilipitisha majina mapya ya wagombea uenyekiti, Elias Mbao, Godwin Mkanwa na Joseph Mwalimu. Henry Mwenge na Prosper Mutungi wamepitishwa kuwania Ukatibu wa Itikadi na Uenezi mkoa.
Kwa mkoa wa Geita, sura mpya zilizopitishwa kuwania nafasi hiyo ni Alhaji Kalidushi, Simon Mayengo na John Luhemeja. Upande wa Katibu wa Siasa na Uenezi waliopitishwa ni David Azaria na Zacharia Bwire. Kwa mkoa wa Iringa waliopitishwa ni Evans Balama ambaye ni mkuu wa zamani wa wilaya, Albert Chalamila na Daniel Kidava.
Waliopitishwa uenezi ni Mwinyiheri Baraza na Josia Kifunge. Mkoa wa Katavi wagombea wapya ni Enock Gwambasa, Beda Katani na Philip Kalyalya. Wanaowania Ukatibu wa Siasa na Uenezi ni Linus Kasakabaya na Jackson Lema. Mkoa wa Kilimanjaro, wagombea wapya wa uenyekiti ni Alfonse Temba, Patrick Boisafi na Daudi Mrindoko .
Waliopita Ukatibu, Siasa na Uenezi ni Mahamoud Karia, Juliana Mamuya na Rodger Msangi. Mwenyekiti wa Manyara, wagombea wapya ni Simon Issay, Fratern Kwahhison na Alais Mbarnot.
Jacob Aloyce na Gabriel Bukhay watachuana uenezi. Kwa mkoa wa Mbeya, NEC ilipitisha sura mpya, Dk Momole Kasambala, Jacob Mwakasole na Andilile Mwambalaswa. Katibu wa Siasa na Uenezi waliopitishwa ni Gordon Kalulunga, Philemon Ng’ong’o na Bashiru Madodi.
Mtwara, ni Moza Nguruwe, Yusuph Nannila na Rajabu Kazibure. Waliopitishwa Ukatibu, Siasa na Uenezi ni Halfani Matipula na Paul Ndomba. Njombe ni Joseph Mwamala, Nikolaus Ng’eve na George Mng’ing’o. Walioteuliwa Ukatibu Siasa na Uenezi ni Erasto Ngole na Ananias Kitola.
Shinyanga, ni Mabala Mlolwa, Cornel Ngudungi na John Makune. Wanaowania Ukatibu wa Siasa na Uenezi ni Msanii Masele Emmanuel, Mlimandago Jonas Musa na Jakrine Brayi.
Simiyu, NEC ilimrejesha Mwenyekiti wa sasa, Dk Titus Kamani, Enock Yakobo na Jonathan Mnyela. Ukatibu wa Siasa na Uenezi ni Kagya Enock, Danhi Makanga, Zaina Mbaruk na David Sendo.
Singida waliopitishwa uenyekiti ni Yusuph Gwayaka, Juma Kilimba, Hussein Kilongo na Celestine Yunde. Mwenyekiti wa zamani, Mgana Msindai alihamia Chadema kabla ya kurudi.
Ukatibu Uenezi ni Ahmed Athuman na Musa Nkungu. Mkoa wa Songwe, walioteuliwa uenyekiti ni Ellynico Mkola, Hezron Mwashibanda na Ramadhan Msaka. Katibu uenezi na siasa walioteuliwa ni Neema Nzowa na John Zumba.
Mkoani Mara, nafasi ya uenyekiti ni, Chirangi Msuto, Namba Samuel na Rayah Thobias. Tabora NEC imempitisha mgombea pekee, Mwenyekiti wa sasa, Hassan Wakasuvi. Kwa upande wa Katibu wa siasa na uenezi waliopitishwa ni Luboya Kadegele na Ismail Bilali.
Mwenyekiti Costancia Buhiye wa Kagera amerejeshwa kutetea nafasi hiyo. Waliopitishwa kuchuana naye ni Medard Mushobozi na Christopher Kiiza. Mkoani Tanga, walioteuliwa Uenyekiti ni Mohamed Risherd Abdalah, Balozi Abdi Mshangama na Henry Shekifu anayetetea nafasi yake.
Ukatibu wa Siasa na Uenezi waliopitishwa ni Prudence Kibuka, Sajida Abeid na Hamimu Omary. Mwenyekiti wa Mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogeris amepitishwa kutetea nafasi yake hiyo huku akipambanishwa na Elia Mpesa na Ally Said.
Mkoani Mwanza, Mwenyekiti wa sasa, Dk Anthony Diallo atatetea nafasi yake akipambanishwa na Enock Masele, Richard Rukambula na Said Mecky Sadiki ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro.
NEC pia ilipitisha majina ya wanaowania nafasi 15 za ujumbe wa NEC Taifa Tanzania Bara maarufu Kundi la Kapu. Miongoni mwa waliopitishwa ni William Sarakikya, Angela Akilimali, Dk Fenella Mukangara, Jerry Silaa, Stephen Wassira, Ernest Sungura, Richard Bundala, Alfred Lawrence, Praxeda Mazimba, William Simwali, Method Mselemwa na Mwantumu Zodo. Wanaowania Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ni Dk Edmund Mndolwa, Burton Kihaka, Simon Rubugu na Fadhil Maganya.
•Tuma habari picha na video za matukio mbalimbali WhatsApp kwa 0625966236
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: