Shilingi elfu kumi ya Tanzania
Benki kuu ya Tanzania inasema kuwa imeipokonya leseni ya kuhudumu benki ya FBME ya Tanzania baada ya kushutumiwa na serikali ya Marekani kwa utakatishaji wa fedha haramu, kulingana na chombo cha habari cha Reuters.
Benki hiyo iliosajiliwa nchini Tanzania ilikabiliana kisheria dhidi ya madai hayo ,lakini mahakama moja ya Marekani ilitoa uamuzi uliopendelea idara ya fedha ya Marekani kwa kuchukua hatua hiyo.
Kulingana na benki kuu ya Tanzania mnamo tarehe 24 Julai 2014 Benki Kuu ya Tanzania iliiweka chini ya usimamizi maalumu (statutory management) benki ya FBME Bank Limited (FBME).
Hatua hii ya Benki Kuu ilitokana na Notisi iliyotolewa tarehe 15 Julai 2014 na Taasisi ya Marekani inayopambana na Uhalifu wa Kifedha "the US Financial Crimes Enforcement Network" kwa kifupi FinCEN, iliyoituhumu FBME kuwa ni taasisi inayojihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu
Uamuzi huo wa mahakama unaongeza athari kwa kiwango kikubwa katika uendeshaji wa FBME kwa kuwa haitaweza tena kufanya miamala ya kibenki ya kimataifa na kupata huduma za mifumo ya kibenki na hivyo itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wateja wake kwa mujibu wa leseni waliyopewa.
Katika taarifa, benki kuu ilisema kuwa imesitisha huduma zote za benki ya FBME na imeiweka chini ya ufilisi
Reuters inasema kuwa FBME haikutoa mara moja tamko lake kuhusu hatua hiyo.
Benki ya FBME imesajiliwa katika taifa hilo la Afrika mashariki lakini imekuwa ikitekeleza huduma zake katika maeneo mengine hususan nchini Cyprus.
0 Post a Comment:
Post a Comment