Rais wa Uchina amelalamikia hatua ya Marekani kuweka mtambo wa kuzuia makombora nchini Korea Kusini.
Rais Xi Jinping amepinga kuwepo kwa mtambo huo katika mazungumzo yake ya kwanza na rais mpya wa Korea Kusini Moon Jae-in.
Mtambo huo wa Thaad, ambao lengo lake ni kutungua makombora ambayo huenda yakarushwa na Korea Kaskazini, ulianza kufanya kazi wiki iliyopita.
Beijing hata hivyo inasema mtambo huo unaweza kutumiwa na Marekani kufanya upelelezi katika maeneo ya China na imeupinga sana.
Uhusiano kati ya Beijing na Seoul umeathirika sana kutokana na kuwekwa kwa mtambo huo.
Bw Moon alichaguliwa kuwa rais mpya wa Korea Kusini siku ya Jumanne.
Anakabiliwa na changamoto ya kusawazisha uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani, mshirika wa tangu zamani wa Seoul, pamoja na uhusiano wake na China - ambayo anahitaji usaidizi wake kukabiliana na Korea Kaskazini na mpango wake wa kuwa na silaha za nyuklia.
Msemaji wa rais wa Korea Kusini alsiema kiongozi huyo wa China, ambaye ndiye aliyepiga simu, alieleza sabbau za "Beijing kupinga kwa dhati" kuwepo kwa mtambo huo wa kuzuia makombora.
Shirika la habari la serikali ya Korea Kusini Yonhap limemnukuu msemaji huyo Yoon Young-chan akisema: "Rais Moon amesema suala kuhusu Thaad linaweza likatatuliwa iwapo hakutakuwa na uchokozi tena kutoka kwa Korea kaskazini."
Bw Moon pia aliibua suala la kulipiza kisasi dhidi ya kampuni za Korea Kusini nchini China.
Amesema atatumba ujumbe Beijing kujadiliana na maafisa wa China kuhusu Korea Kaskazini na mpango huo wa Thaad.
Kuwekwa kwa mtambo huo wa Thaad kuliidhinishwa na mtangulizi wa bw Moon, Park Guen-hye ambaye kwa sasa yumo gerezani akisubiri kusikizwa kwa kesi yake kuhusu tuhuma za ufisadi.
Msimamo wa Bw Moon kuhusu Thaad haufahamiki vyema lakini ameonekana kutokuwa na msimmao thabiti awali.
Baadhi ya Wakorea Kusini waliandamana kupinga kuwekwa kwa mtambo huo
Msemaji wake alishtuumu uamuzi wa Marekani kuweka mtambo huo wiki chache kabla ya uchaguzi, akisema hilo lilizuia serikali ambayo ingechaguliwa kupata fursa ya kufanya uamuzi kuhusu mtambo huo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China amesema pande zote mbili zimeeleza nia ya "kuimarisha tena uhusiano kati ya nchi hizo mbili".
Bw Moon na Bw Xi waliafikiana kwamba nchi zote mbili zina lengo la pamoja na kuhakikisha Korea Kaskazini haina silaha za nyuklia.
Bw Moon amekuwa akitaka mazungumzo yatumiwe kutatua mzozo huo, jambo ambalo linatofautiana na mtangulizi wake aliyechukua msimamo mkali zaidi.
THAAD ni nini?
- Ni teknolojia ya kujilinda ya kutungua makombora ya masafa mafupi na wastani ambayo huyaharibu yanapokaribia kulipuka.
- Hugonga kombora la kuliharibu
- Ina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 200 na inaweza kurushwa juu hadi kilomita 150 angani
- Marekani imewahi kuweka mitambo kama hiyo Guam na Hawaii kujilinda dhidi ya uwezekano wa mashambulizi kutoka kwa Korea Kaskazini
0 Post a Comment:
Post a Comment