Dkt Nyanzi akisaidiwa kutembea na maafisa wa mahakama
Mwanaharakati msomi nchini Uganda ambaye alikamatwa baada ya kumuita Rais Yoweri Museveni "jozi ya makalio", hatimaye amepewa dhamana.
Dkt Stella Nyanzi alifikiwa mahakamani akionekana dhaifu.
Mwandishi wa BBC Patience Atuhaire aliyekuwepo kortini anasema mwanaharakati huyo alizirai alipojaribu kusimama baada ya kikao cha mahakama kuahirishwa kwa muda.
Alisaidiwa kusimama na maafisa wa magereza.
Taarifa zinasema anaugua Malaria.
Upande wa mashtaka ulikuwa umesema iwapo Dkt Nyanzi angepewa dhamana, basi mahakama iweke sharti kuwa achunguzwe afya yake ya kiakili.
Kadhalika, walitaka azuiwe kuandika au kuzungumzia chochote kuhusu Rais, serikali au familia ya Rais.
Mawakili wake hata hivyo walisema anafaa kupewa dhamana kutokana na hali yake ya afya na kwamba anafaa kuruhusiwa kupata nyaraka muhimu kuhusu kesi yake ili kujiandaa kujitetea.
Hakimu aliamua Dkt Nyanzi hafai kujihusisha katika shughuli zozote ambazo zinaweza kuingilia kesi hiyo dhidi yake.
Dkt Nyanzi alikamatwa mwezi Machi baada ya kuandika msururu wa ujumbe kwenye Facebook, ambapo alimshutumu rais Museveni kwa kushindwa kuwapa wasichana kutoka familia maskini vitambaa vya kutumia wakati wa hedhi.
Wasichana wengi nchini Uganda wameripotiwa kuacha masomo kutokana na aibu ya kukosa sodo.
''Ninakataa wazo kwamba mtu hawezi na hafai kukosoa watu wanaonyanyasa haki na mali za Waganda katika miaka 31 ya uongozi wa kidikteta wa familia moja," alisema katika ujumbe wake Facebook wakati huo.
''Kama mtu anayefikiri, msomi, mshairi, mwandishi mmiliki wa akaunti ya facebook na mtayarishaji ni jukumu langu kuwakosoa wafisadi wa siku hizi''.
0 Post a Comment:
Post a Comment