Kila shule ya upili nchini Uganda itapokea nakala mbili za kitabu kuhusu maisha ya Rais Yoweri Museveni cha Sowing the Mustard Seed (Kupanda Mbegu ya Mharadali).
Taarifa kutoka wizara ya elimu nchini humo, ambayo waziri wake ni mkewe Museveni, Janet, inasema kitabu hicho kilichoandikwa na kiongozi huyo kitasaidia "kuendeleza ufahamu na kuhakikisha uzalendo kwa taifa la Uganda katika juhudi za kuendeleza amani an utangamano wa kitaifa kwa ajili ya maendeleo."
Taarifa hiyo inasema kitabu hicho kinafaa kuwekwa katika kila maktaba ya shule na kwamba wanafunzi wanafaa kuhamasishwa kukisoma.
Kitabu hicho, kwa mujibu wa wizara hiyo, kinasimulia kwa kina chanzo cha historia yenye misukosuko ya Uganda pamoja na kukombolewa kwake na hatimaye safari ya kulikwamua na kuliendeleza taifa hilo.
Kitabu hicho kilichapishwa mwaka 1997, sana kikiangazia msururu wa mahojiano aliyofanyiwa Bw Museveni na mwanahistoria Mwingereza Kevin Shillington.
Bw Museveni, ambaye aliingia madarakani mwaka 1986, kwa sasa anatumikia muhula wake wa tano.
0 Post a Comment:
Post a Comment