1 Mei 2017
Ijumaa iliyopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angellah Kairuki alimkabidhi Rais John Magufuli ripoti ya majina hayo ambayo yameibua mjadala mitaani na mitandaoni.
Akizungumzia suala hilo, Dk Msigwa amesema kama watumishi hao wataendelea kubaki kazini watashtakiwa kwa kughushi vyeti na kujipatia mshahara kinyume na sheria.
“Hapa kuna mtego wahusika wenyewe wataamua kama waendelee na kazi ili waje washtakiwe au kujiondoa mapema na kuacha kiinua mgongo chao,” amesema katibu huyo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kazi na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004, mwajiri anawajibika kumlipa haki zake mfanyakazi pale anapomwachisha kazi.
Hata hivyo, Dk Msigwa amesema Serikali ikiamua kuwafukuza kazi kwa sheria hiyo ni lazima walipwe stahiki zao kwa sababu wameondolewa kwenye ajira kwa lazima.
“Kwa sheria ya kazi namba sita (ya mwaka 2004) hakuna neno kufukuzwa kazi, ukimwondoa kazini mtumishi ni lazima umlipe kiinua mgongo, ndiyo maana hapa ninaona agizo la Rais Magufuli ni mtego ili waache kazi wenyewe,” alisema.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Magufuli aliwataka wafanyakazi hao kuacha kazi ndani ya siku 15 vinginevyo wakumbane na mkono wa sheria baada ya kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua.
0 Post a Comment:
Post a Comment