9 Juni 2017
Mumewe Bi May alikuwa kando yake alipokuwa akihutubia taifa
Hapo awali Waziri Mkuu alitembelea ikulu ya Buckingham
Wanachama wa DUP ambao wanakutana kujadili nafasi yao wanaunga mkono Brexit
Theresa May amesema ataunda serikali iliyo na uhakika wa siku za usoni, akiungwa mkono na chama cha DUP
Akizungumza baada ya kutembelea ikulu ya Buckingham, alisema ni chama chake tu kilicho na "uhalali" wa kutawala, licha ya kushindwa kupata wingi wa wabunge katika uchaguzi wa Alhamisi.
Alisema angeweza kujiunga na "rafiki" zake wa DUP na "kufanya kazi" inayohusiana na Brexit.
Lakini wanachama wa Leba walisema wao ndio "washindi halisi" huku wanademokrasia huria wakisema Bi May unapaswa kuwa na "aibu" ya kuendelea na kazi.
Katika kauli fupi nje ya barabara ya Downing, iliyofuatwa na mkutano wa dakika 25 na Malkia, Bi May alisema ana nia ya kuunda serikali ambayo inaweza "kutoa uhakika na kuipeleka Uingereza mbele kwa wakati huu muhimu kwa nchi".
Akizungumzia "uhusiano imara" aliokuwa nao na DUP lakini akitoa maelezo kidogo ya jinsi mpangilio wao unaweza kufanya kazi, alisema serikali itaweza "kuongoza nchi katika mazungumzo muhimu ya Brexit" yanayofaa kuanza katika muda wa siku 10 tu.
"Vyama vyetu viwili vimekuwa na uhusiano bora kwa miaka mingi," alisema.
"Na hii inanipa mimi imani ya kwamba tutaweza kufanya kazi pamoja kuboresha maslahi ya Uingereza."
Kiongozi wa DUP Arlene Foster alithibitisha kwamba amezungumza naye Bi May na kuwa watawasiliana zaidi ili "kujadili jinsi wataweza kuleta utulivu kwa taifa, wakati huu wa changamoto kubwa".
Licha ya kuwa wanafanya bidii siku zote kwa ajili ya "mpango bora" kwa Ireland ya Kaskazini na watu wake, alisema chama chake daima kinataka manufaa yaliyo bora kwa Uingereza kwa jumla.
Baada ya matokeo ya maeneo mengi kutangazwa, Theresa May alipungukiwa na wabunge 12 ukilinganisha na wabunge aliokuwa nao wakati wa kuitisha uchaguzi huo.
Kiongozi wa chama cha Leba Jeremy Corbyn amesema pia kwamba yuko "tayari kutumikia".
Mhariri wa masuala ya siasa wa BBC Laura Kuenssberg amesema Bi May anakusudia kujaribu kuongoza kwa msingi ya kwamba chama chake kilipata idadi ya juu zaidi ya kura na wabunge wengi.
Conservatives walipoteza viti 13. Chama cha SNP nacho kilipoteza viti 22, ambavyo vimetwaliwa na Conservative, Labour na Lib Dems, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa kiongozi wa chama hicho Nicola Sturgeon.
Idadi ya waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo wa Alhamisi kufikia sasa ni 68.7% - juu na 2% ukilinganisha na 2015 - lakini uchaguzi huo umepelekea kurejea kwa siasa za vyama viwili katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Vyama vikuu viwili - Conservative na Labour - vimepata idadi kubwa ya kura kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1990.
Chama cha UKIP kilipoteza kura nyingi , lakini badala ya kura hizo kuendea chama cha Conservative kama walivyotarajia, wapiga kura wengi waliokuwa wanaunga chama hicho walihamia chama cha Labour.
Bw Corbyn, akizungumza baada ya kuchaguliwa tena Islington North, alisema wakati umefika kwa Bi May "kufungua njia kuwezesha kuundwa kwa serikali ambayo itawakilisha kikamilifu maslahi ya nchi hiyo.
Baadaye, aliambia BBC kwamba ni wazi kabisa nani alishinda uchaguzi huo.
"Tuko tayari kuwatumikia wananchi ambao wameweka imani yao kwetu," alisema, lakini akasisitiza kwamba hataingia kwenye mkataba na vyama vingine.
Chama cha Conservatives kimesema iwapo kutakuwa na bunge la mng'ang'anio atapata nafasi ya kuunda serikali kwanza, kama ilivyofanyika mwaka 2010 mtangulzii wake David Cameron alipokosa wingi wa wabunge.
0 Post a Comment:
Post a Comment