27 Sep 2017
Sababu kubwa inayotajwa kuifanya shule hiyo, iliyojengwa na wakoloni wa Kijerumani miaka ya 1800, ikose walimu wa kike ni kadhia za mazingira ya kazi zinazochochewa na ugumu wa kufikika kutoka makao makuu ya Wilaya ya Nkasi, Namanyare.
Wanafunzi 10 wa kike wa Shule ya Msingi Mandakerenge iliyopo zaidi ya kilomita 30 kutoka Namanyere wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa wanaingia katika ofisi ya mwalimu mkuu wakiwa wamembeba mwenzao aliyezimia.
Wanamuweka chini na kuanza kumpepea ili azinduke. Mwalimu mkuu msaidizi, Yona Nkwamba anatoa nafasi kwa wanafunzi hao kumuhudumia mwenzao.
Ni kawaida kwa wanafunzi hao wa shule hiyo iliyopo katika Kisiwa cha Mandakerenge kuhudumiana katika masuala yanayohusu jinsi yao yakiwemo hedhi kwa kuwa hakuna mwalimu wa kike ambaye angewahudumia kama ilivyo kwa shule nyingine nchini.
Kukifikia kisiwa hicho ni lazima uikate barabara ya vumbi kutoka Namanyere inayoelekea pwani ya Ziwa Tanganyika ambako vipo visiwa vingine vyenye changamoto lukuki kiasi cha kutishia baadhi ya watumishi wa umma kwenda kufanya kazi.
Usafiri katika barabara hiyo inayopita kwenye mabonde na milima kuelekea vijiji vya Katongolo na Kipili unapatikana mara moja asubuhi na jioni.
Unapofika Kijiji cha Kipili ambako kumechangamka, bado kuna safari ya kufika ziwani ambako kuna mitumbwi ya kienyeji ya kukupeleka visiwani.
Japo kuna mtumbwi wenye injini unaofanya safari kati ya visiwa vya Mvuna, Mandakerenge na mji wa Kirando ambao hupita asubuhi na jioni, bado watu wengi hutumia mitumbwi ya kupiga makasia jambo ambalo ni hatari kiusalama.
Mandakerenge kimejaa miamba na mawe mengi na hakina barabara, hivyo kukifanya kisifikike kwa urahisi kutokana na kukosa miundombinu ya kuwezesha kupita magari, pikipiki wala baiskeli. Njia rahisi ya kuvifikia vitongoji vya kijiji cha kisiwa hicho ni kutembea kwa miguu au kutumia mitumbwi kwa kuzunguka ziwani.
Mazingira hayo ndiyo yamesababisha Shule ya Msingi ya Mandakerenge kukosa kabisa walimu wa kike kwa karibu miaka 30 sasa na kuwafanya watoto wa kike wakose huduma muhimu ambazo zingetolewa na watumishi wa kike hususan wanapokuwa katika hedhi.
Sababu kubwa inayotajwa kuifanya shule hiyo, iliyojengwa na wakoloni wa Kijerumani miaka ya 1800, ikose walimu wa kike ni kadhia za mazingira ya kazi zinazochochewa na ugumu wa kufikika kutoka makao makuu ya Wilaya ya Nkasi, Namanyare.
Malalamiko ya wanafunzi
Esther John anayesoma darasa la saba katika shule hiyo anasema wangetamani kupata walimu wa kike ili wawaeleze shida zao zinapowakuta lakini inashindikana kwa sababu walimu wote ni wanaume.
“Wakati mwingine tunakuwa na shida zinazotuhusu wasichana kama kuwa na hedhi lakini hatuwezi kuwaeleza walimu wa kiume. Tunapenda hata kuelimishwa mambo ya wanawake, lakini hatuna mtu wa kutufundisha. Wenzetu wavulana wanafaidika zaidi,” anasema Esther.
Wengine ambao hawawezi kujisitiri wenyewe wakiwa shule kama Mwajuma Hamza hulazimika kurudi nyumbani huku wakiacha masomo yakiendelea.
Mwajuma anayesoma darasa la sita anasema wanapokuwa na shida za hedhi kama imewatokea wakiwa nyumbani huairisha shule ili wasaidiwe makwao na mama au walezi wao wa kike.
“Tunapopata shida kama hedhi, tunaaga na kurudi nyumbani, walimu wanatuelewa kwa sababu hakuna mwalimu wa kike hapa. Tungepetamani kupata walimu wa kike ili watusaidie zaidi tukiwa shule,” anasema Mwajuma.
Wazazi wakabiliana na hali
Elizabeth Mnazi, mzazi ambaye mtoto wa kike anasoma shule hiyo, anasema wanajua changamoto hiyo ya uhaba wa walimu wa kike ndiyo maana huwa karibu na watoto wao kuwasaidia.
“Ni kweli shule haina walimu wa kike, lakini ikitokea shida watoto wanarudi nyumbani haraka. Ikiwa kuna ulazima wa kwenda shule tunakwenda kuwachukua. Tumeshaueleza uongozi wa kijiji, lakini tumeambiwa ni mpaka Serikali iajiri walimu,” anasema Elizabeth.
Mwalimu mkuu msaidizi, Nkwamba anasema mazingira magumu ni sehemu ya kazi na ikitokea shida kwa wasichana huwa wanawaruhusu waende nyumbani haraka.
Anasema tatizo kubwa linalowakabili kiasi cha kuchangia walimu wanawake kukimbia ni ukosefu wa nyumba bora za kuishi.
“Kuna jumba moja tumepanga halina madirisha wala milango ndiyo tunaishi humo kwa kutenganishwa na mapazia,” anasema Nkwamba.
Kuhusu vifaa, Nkwamba anasema awali hakukuwa na madawati ya kutosha, lakini kwa kampeni iliyofanywa na Rais John Magufuli wamepata madawati mengi japo bado kuna uhaba wa madawati 53.
“Inabidi darasa la kwanza wasome kwa zamu ili madawati yatoshe. Vitabu hasa vya sayansi havipo kabisa licha ya Serikali kubadilisha mtaala, inabidi tufundishe kwa uzoefu tu,” anasema.
Shule hiyo inakosa walimu wa kike licha ya takwimu za msingi za elimu za mwaka 2016 (BEST 2012-2016) zilizotolewa na Ofisi ya Rais-Tamisemi hadi mwaka jana kubainisha kuwa shule za awali, msingi na sekondari nchini zilikuwa na walimu wa kike wengi zaidi wapatao 106,085 ikilinganishwa na walimu wa kiume 100,744.
Diwani wa Kata ya Kipili, Wilbrod Chakukila aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo tangu mwaka 1993 anasema Serikali imeshindwa kupeleka walimu wa kike kisiwani humo akitaja ushirikina kuwa moja ya sababu mbali na mazingira magumu.
“Nimezaliwa katika kisiwa hiki na nimekuwa mwalimu wa shule hii kwa zaidi ya miaka 20 hadi nilipostaafu. Mwaka 1993 walimu wote zaidi ya 10 waliokuwa wakifundisha shule hii waliacha kazi wakidai kuwa wanarogwa. Shule ikabaki bila walimu,” anasimulia Mwalimu Chakukila.
“Ilibidi Serikali itafute walimu ambao ni wazawa wa maeneo haya. Mimi nilikuwa nafundisha huko Sumbawanga, nikaitikia wito wa kurudi nyumbani na baadhi ya walimu, lakini walimu wa kike walikataa. Tangu wakati huo nikawa mwalimu mkuu hapa.”
Anasema kutokana na kukosekana walimu wa kike, kumekuwa na changamoto za kuwasaidia wanafunzi wa kike hasa wa madarasa ya juu waliovunja ungo wanapopata hedhi.
“Kuna changamoto kubwa wanapoingia mwezini, inabidi tu utumie wanafunzi wenzao kuwasaidia na kuwarudisha nyumbani. Walimu wa kike wangeweza kuwasaidia na kuwatia moyo, lakini ndiyo hawapo,” anasema na kuongeza:
“Ilinitokea mara kadhaa nikiwa mwalimu shuleni hapo. Kuna wakati nikiwa nafundisha mtoto wa kike aliugua ghafla, kwa kuona aibu ikabidi niwatoe nje wavulana wote nikawaambie wakanisubiri ofisini kwangu, wakati huo wanafunzi wa kike walimsafisha na kumpeleka kwao mwanafunzi huyo wa kike.”
Mbali na walimu wa kike, Chakukila anasema kwa ujumla mazingira ya kisiwa hicho ni magumu kuzoeleka kwa wageni na hivyo kuchangia walimu wengi kushindwa kufanya kazi.
“Walimu wanapenda mazingira yenye motisha ili kuongezea kwenye mshahara ulio mdogo. Sasa umlete mwalimu hapa, kisiwa chote ni mawe matupu, hakuna barabara hivyo hakuna gari wala pikipiki. Mwalimu hata akija hapa atakaa mwaka mmoja kisha anaondoka kwa visingizio vingi,” anasema.
“Walimu wa kiume wanaishi hapa kwa ugumu tu, kwa ujumla Serikali imeshindwa kuleta walimu wa kike huku.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Clarence Msemakweli anasema shule hiyo ina wanafunzi 622 ambapo kati yao wasichana ni 308 na wavulana ni 414 ina walimu saba wa kiume na upungufu wa walimu sita.
Tatizo la uhaba wa walimu wa kike linaathiri wilaya baada ya takwimu kutoka katika halmashauri hiyo kuonyesha kuwa kati ya walimu 171 walioajiriwa na kuripoti mwaka 2015 ni walimu 39 ndiyo walikuwa wanawake.
Hii ina maana kuwa kwa kila walimu 10 walioripoti, ni watatu tu walikuwa wanawake.
Wilaya hiyo ina upungufu wa walimu wa shule za msingi kwa asilimia 38 baada ya kuwepo walimu 1,084 kati ya 1,696 wanaojihitajika.
Wadau wa afya na watetezi za haki za wasichana wanasema kuwa ukosefu wa ushauri wa masuala ya maumbile kwa watoto wa kike una athari katika makuzi na afya zao.
Ofisa wa Sera na Utetezi wa Mtandao wa usafi wa mazingira na maji (Tawasanet), Darius Mhawi anasema kuna tatizo kubwa la afya ya wasichana wanaopevuka kwa kukosa huduma na ushauri wa kujitunza.
“Sisi ni wadau na role (jukumu) yetu ni kufanya utafiti na kuishauri Serikali kuhusu usafi wa mazingira. Tulifanya utafiti katika wilaya za Temeke kwa maeneo ya mijini na Kilomero kwa maeneo ya vijijini. Nadhani tatizo la Nkasi litakuwa linafanana na changamoto tulizoziona vijijini,” anasema.
“Tumeishauri Serikali kuongeza usimamizi na utoaji wa pedi za kike kwa wanafunzi, kuboresha vyoo vya wanafunzi, kuweka huduma ya maji na matibabu kwa sababu wengine wakiwa kwenye hedhi wanapata maumivu. Vilevile tumewahusisha wabunge akiwemo Sophia Mwakagenda ambaye ni mhamasishaji wetu kinara,” anaongeza Mhawi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo anasema tatizo la walimu wa kike siyo kwa shule hiyo pekee, bali ni kwa wilaya nzima na wanafanya mikakati ya kuongeza walimu.
“Siyo kweli kwamba walimu hawataki kwenda vijijini, ila wilaya ya Nkasi yote ina uhaba mkubwa wa walimu hasa wa kike. Nimetoka mkoani Dodoma hivi karibuni ambako tumejadili tatizo hilo na Serikali imeahidi kutuongeza walimu wakiwemo wa kike,” anasema Kaondo.
TUFUATE FACEBOOK:ZAKACHEKA.HABARI
0 Post a Comment:
Post a Comment