27 Sep 2017
Sheria mpya na ukaguzi wa makampuni ya uchimbaji madini nchini Tanzania zimepunguza uwekezaji katika sekta hiyo.
Sheria hizo mpya ziliidhinishwa kufutilia mbali kile ambacho rais Magufuli amekitaja kuwa miaka mingi ya mienendo ya kifisadi na ukwepaji kulipa kodi, iliochangia taifa hilo kupoteza mapato kutoka sekta inayochangia kiasi cha asilimia 4 ya pato jumla nchini.
Rais Magufuli aliidhinisha mwezi Julai sheria mpya ya madini inayoipa serikali 16% ya miradi yoyote ya uchimbaji madini.
Athari ni kubwa kiasi gani
Baadhi ya makampuni yanayo jihusisha na masuala ya uchimbaji madini Tanzania yametoa taarifa za aidha kupunguza shughuli zao za uzalishaji au hata nguvu kazi.
Huku makampuni mengine yakisitisha kabisa shughuli zao.
Rais Magufuli amesema haogopi kufunga shughuli zote za uchimbaji madini nchini ili kuisahihisha hali.
Amesema, "Iwapo ni kuanza upya basi tufanye hivyo. Na iwapo madini yetu mengi yameibiwa basi na tuyafunge migodi.
"Pengine watoto wetu na wajukuu wetu watakuwa na akili zaidi na watakuja kuifanya biashara hii badala ya kutazama tu madini haya yakiibiwa."
Mawaziri wa zamani na wa sasa na maafisa wengine serikalini, wametajwa na kutuhumiwa kushirikiana na makampuni hayo ya uchimbaji madini na kusaini kandarasi zinazotiliwa shaka.
Faida au Hasara
Wadadisi wanatathmini kuwa athari ya wazi iko kwa nguvu kazi, wafanyakazi wanaopunguzwa katika baadhi ya makampuni yanayo punguza au kusitisha shughuli zao.
Wanakosa ajira katika maeneo waliotegemea kupata kipato chao kujikimu ki maisha.
Kwa upande wa serikali, mtazamo ni kuwa hakuna kinachopotea.
Said Msonga mtaalamu wa masuala ya uongozi na mahusiano ya kimataifa anaeleza,
'Inaipa nafasi zaidi serikali kudhibiti sekta hii na kujipatia kipato zaidi ambacho hapo zamani kilikuwa kinapotea katika mazingira ya udhaifu wa sheria zilizokuwepo'.
Wasiwasi ni upi kwa wawekezaji:
Sheria mpya zilizoidhinisha ambazo kwa namna moja ama nyingine zimezidisha udhibiti katika biashara ya madini, zimesababisha fikra kwa baadhi ya wadau katika sekta hiyo kwamba namna ambavyo shughuli zitakavyokuwa zikijiendesha hazitawapa faida walioitarajia.
Na ndio sababu ya kufikia maamuzi kama hayo ya kupunguza shughuli katika kukabiliana na matakwa ya kisheria, au wengine kulazimika kusimamisha shughuli zao.
Na hususan kwa kulinganisha faida ya siku za nyuma na hali itakavyokuwa baada ya kuwepo sheria za udhibiti.
Kampuni ya Acacia ilituhumiwa kwa ukwepaji wa kulipa kodi ya thamani ya $180bn, imekana hilo
Muda wa Uangalizi:
Kwa wawekezaji wapya huu ni muda wa uangalizi.
Wanapitia sheria hizo kwa kina na matakwa yake katika kuona namna ambavyo wanaweza kufanya uwekezaji wao ukawa ni wa faida katika mazingira ya kisheria.
Hatahivyo wanauchumi wanaona athari kubwa inawaendea wale ambao tayari walikuwa wana shughuli zao Tanzania kuliko ambao hawajajikita na kuanza shughuli hizo.
Ingawa bado ni mapema kuweza kupima kiwango cha ufanisi kutokana na kwamba ni muda mfupi tangu kuidhnishwa sheria hizo, baadhi ya wadadisi ndani ya Tanzania wanaona pengine serikali ingechukua hatua hizi mapema zaidi, kwa maslahi mapana ya taifa hilo.
Lakini pia wakosoaji wanaona ni hatua isiyozingatiwa maslahi ya upande wa pili katika kutatua tatizo hilo, na huenda ikatishia wawekezaji zaidi wa nje.
0 Post a Comment:
Post a Comment