Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba kuwapatia walimu silaha kunaweza kuzuia mashambulio ya risasi katika shule kama lile lililowaua watu 17 wiki iliopita mjini Florida.
''Mwalimu mwenye bunduki anaweza kukabiliana na washambuliaji mara moja'', alisema. Bwana Trump alitoa pendekezo hilo huku manusura wa shambulio hilo la tarehe 14 mwezi Februari wakimtaka kuhakikisha kwamba shambulio kama hilo halitokei tena.
Rais huyo wa Republican pia aliunga mkono wito wa kuwakagua wanakotoka wanunuzi wa bunduki. Manusura wengine wakati huohuo waliwataka wa bunge wa Florida kuweka udhibiti wa bunduki.
''Tutakuwa thabiti iwapo kutakuwa na ukaguzi mbali hali ya kiakili ya mtu anayetaka kumiliki bunduki''. Trump aliwaambia wanafunzi kutoka shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas wakati wa hafla hiyo iliorushwa hewani moja kwa moja katika ikulu ya Whitehouse.
''Haitakuwa maneno kama ilivyokuwa awali'', aliongezea. Rais huyo wa Marekani pia aliunga mkono pendekezo lililoungwa mkono na muungano wa wamiliki wa bunduki NRA .
Aliaahidi kuangazia kuhusu wito kwa walimu kupewa bunduki. ''Iwapo una mwalimu ambaye ana bunduki'', alisema ''anaweza kusitisha shambulizi lolote kwa haraka. Iwapo mwalimu angemiliki bunduki , ijapokuwa najua ni swala ambalo lingezua utata, wangepewa mafunzi maalum na wangesaidia pakubwa''.
''Kusingekuwa na uhuru wa kuingia katika shule na kuanza kufyatua risasi, kwa sababu washambuliaji wangekuwa waoga''.
Majimbo kadhaa ya Marekani tayari yanaruhusu bunduki ndani ya vyuo na taasisi za elimu kulingana na tovuti ya kujihami katika vyuo. Jimbo la Florida hatahivyo halifanyi hivyo.
Rais huyo wa Marekani alisikiliza malalamishi ya mabadiliko ya sheria za umiliki wa bunduki siku ya Jumatano kutoka kwa wanafunzi 40 , walimu na familia.
Baadhi ya wale waliohudhuria hafla hiyo ya saa moja waliunga mkono wazo la rais Trump kuwahami walimu.
Lakini Mark Barden ambaye mwanawe aliuawa katika shambulio la 2012 katika shule ya Sandy Hook Elementary School mjini Connecticut - anasema ''ongezeko la bunduki sio suluhu. Walimu wana majukumu zaidi kwa sasa kwa wao kuchukua jukumu jingine la kutumia nguvu ili kumuua mtu'', alisema.
0 Post a Comment:
Post a Comment