Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wameendelea kutumia muda wao mwingi kulalamika kile wanachokiita kuminywa katika kufanya shughuli zao za kisiasa.
Wakati huo huo, wanasiasa hawa wamejikuta upande mbaya wa sheria ambapo wapo wengi hivi sasa wanaozongwa na utitiri wa kesi.
Kinachoendelea kuwashangaza wengi pia si tu idadi ya kesi zinazowakibili, lakini pia idadi ya wanasiasa wanaokabiliwa na kesi hizo. Wengine hata wanatakiwa kuhudhuria katika vituo vya polisi kila siku.
Lakini ni kesi gani hizi zinazowaandama wanasiasa hawa?
Zitto Kabwe, kiongozi mwandamizi wa chama cha ACT-Wazalendo amekuwa ni miongoni mwa watu waliojikuta matatani kwa misingi ya sheria ya makosa ya takwimu. Sheria hii imekuwa ikipingwa vikali na wanaharakati kuwa ni kandamizi kwa watoaji na wapokeaji wa taarifa.
Lakini hivi karibuni wakati Kabwe alipokuwa katika ziara ya kichama katika mikoa mbali mbali nchini Tanzania, alijikuta matatani na vyombo vya usalam kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kosa la kufanya mikutano ya kisiasa bila kuwa na kibali rasmi cha polisi.
Chama kikuu cha upinzani Chadema ndicho kinachoonekana kuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wake wanaozongwa na kesi mbali mbali.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, kuna wabunge 13 wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali.
Mbunge wa Singida, kupitia chama cha chadema Tundu Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu,anakabiliwa na kesi sita. Kesi zote zinahusiana na uchochezi.
Lissu anasemekana kuwa ndiye mwanasiasa aliyekamatwa mara nyingi zaidi ya wengine. Miongoni mwa kesi zake zilizoibua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi ni ile aliyoshutumiwa kutoa matamko ya uchochezi na kumuita Rais John Magufuli 'dikteta uchwara'.
Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la kazi zake za usanii Sugu, ambaye ni mbunge wa Mbeya mjini, sasa yuko gerezani kwa kipindi cha miezi mitano baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kutumia lugha za matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Kwa upande wake Halima Mdee, mbunge wa jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, yeye anazo kesi nne zote zikiwa za uchochezi ikiwemo ile aliyotuhumiwa kutumia lugha mbaya kumpinga Rais Magufuli baada ya kutangazwa kwa marufuku ya kuwaruhusu wanafunzi wa kike kurudi shuleni mara wapatapo ujauzito.
Mbunge wa Arusha Godbless Lema yeye anakabiliwa na kesi nne pia huku zote zikiwa za uchochezi. Siku za nyuma Lema aliwahi kukaa mahabusu kwa muda wa miezi minne kwa kosa la uchochezi. Hivi sasa Lema amekuwa akihudhuria mahakamani mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Chadema taifa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe yeye ana kesi mbili. Kwa sasa anahitajika kuhudhuria polisi kila siku.
John Mnyika mbunge wa jimbo la ubungo jijini Dar es salaam kwa upande wake anahitajika kuhudhuria polisi kila wiki tangu jaribio la kufanyika kwa maandamano ya chama hicho mwezi uliopita. Huyu kesi yake yeye bado haijawekwa wazi
Mbunge wa Mara, Esther Bulaya, aliwahi kushikiliwa na polisi kwa kosa la kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake, jambo ambalo polisi walidai kuwa lilikuwa ni uvunjifu wa sheria.
Licha ya kuwa wanaharakati na asasi za kutetea haki za binadamu kuwa mstari mbele kuwatetea wanasiasa hao bado serikali hiyo imekuwa ikibaki kwenye msimamo wake kuwa wanasiasa hao wanavunja sheria.
0 Post a Comment:
Post a Comment