Prof Stephen Hawking, mwanafizikia maarufu duniani, amefariki dunia akiwa na miaka 76, familia yake imetangaza.
Mwingereza huyo alifahamika sana kwa kazi yake ya kisayansi kuhusu uwepo wa eneo katika anga za juu ambapo nguvu za mvutano huwa za juu sana kiasi kwamba miali nururishi au hata mwanga hauwezi kuponyoka.
Kwa Kiingereza, eneo hilo hufahamika kama 'Black Hole'.
Alitumia hilo katika kujaribu kufafanua kuhusu asili ya vitu vyote duniani na angani.
Alikuwa mwandishi wa vitabu kadha maarufu vya sayansi kikiwemo A Brief History of Time (Historia Fupi kuhusu Wakati).
Watoto wake, Lucy, Robert na Tim, wamesema: "Tumehuzunishwa sana kwamba baba yetu mpendwa ametuacha."
"Alikuwa mwanasayansi muhimu na mtu wa kipekee ambaye kazi zake na mchango wake vitaendelea kukumbukwa kwa miaka mingi."
Mambo muhimu kuhusu maisha yaStephen Hawking
- Alizaliwa 8 Januari 1942 Oxford, England
- Alipata nafasi chuo kikuu cha Oxford kusomea sayansi ya mambo asilinia mwaka 1959, kabla ya kwenda kusomea shahada ya uzamifu chuo kikuu cha Cambridge
- Kufikia 1963, alipatikana na ugonjwa ulioathiri mfumo wake wa neva na mawasiliano mwilini. Madaktari walimwambia hangeishi zaidi ya miaka miwili.
- Alieleza nadharia yake kwamba 'black hole' kutoa "Miali ya Hawking" mwaka 1974
- Alichapisha kitabu chake A Brief History of Time mwaka 1988. Nakala zaidi ya 10 milioni za kitabu hicho ziliuzwa.
- Maisha yake yaliangaziwa kwenye filamu ya The Theory of Everything ya mwaka 2014 ambapo Eddie Redmayne aliigiza nafasi ya mwanasayansi huyo
Stephen Hawking alipokuwa na miaka 22 pekee aliambiwa na madaktari angeishi miaka mingine miwili pekee baada yake kupatikana na ugonjwa nadra sana wa mfumo wa neva.
Ugonjwa huo ulimfanya kulemaa na kulazimika kutumia kiti cha magurudumu.
Nyakati za mwisho za maisha yake, alikuwa hawezi kuzungumza ila kwa kutumia kifaa cha kufasiri mawazo yake na kuyageuza kuwa sauti.
0 Post a Comment:
Post a Comment