Kuibuka kwa ufa mkubwa katika eneo la Suswa katika Bonde la Ufa kusini magharibi mwa Kenya kumezua wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo la Afrika Mashariki kijiolojia.
Wataalamu wanasema kutokea kwa ufa huo katika jimbo la Nakuru ni shughuli ya kijiolojia inayochukua muda mrefu ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda.
Hilo limezua hatari ya kuanza kutokea tena kwa mitetemeko ya ardhi na milipuko ya vilkano.
Wanajiolojia wanasema baada ya mamilioni ya miaka, bara la Afrika litapasuka na kuwa vipande viwili.
Sehemu ya mpasuko itakuwa kwenye Bonde la Ufa jambo ambalo linazua uwezekano wa Kenya na Tanzania, pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kujitenga na bara la Afrika.
Mwanajiolojia David Adede ameambia BBC kwamba ufa huo ni sehemu ya kutengana kwa vipande viwili vikubwa vya bara Afrika ambako kutasababisha bara Afrika kutengana na kuwa mabara mawili.
Amesema shughuli hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda lakini dalili zake zilikuwa zinafichwa na majivu ya volkano ambayo polepole yamekuwa yakiziba ufa kila unapotokea.
"Maji ya mvua yamesomba majivu hayo pamoja na mchanga na kuufanya ufa huo kuonekana zaidi," amesema.
Anasema vipande hivyo vimekuwa vikitengana "katika kasi ya sentimita mbili kila mwaka."
Kipande kilicho na sehemu kubwa ya bara hufahamika kama Kipande cha Nubia na kipande cha pili hufahamika kama Kipande cha Somalia.
Dkt James Hammond kutoka kwa Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Dunia kutoka chuo cha Imperial College London alinukuliwa na jarida la mtandaoni la Mail & Guardian akisema: "Katika miaka milioni kadha ijayo, shughuli hii itakamilika na kuigawa Afrika mara mbili, na kuunda bahari mpya hapo katikati na bara jingine. Ukitumia jiografia ya sasa, bara hilo jipya litashirikisha Somalia, nusu ya Ethiopia, Kenya na Tanzania."
Baadhi ya wanajiolojia wanakadiria kwamba huenda mpasuko huu ukayabeba pia mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na maeneo ya Malawi na Msumbiji.
Mwanajilojia Dereje Ayalew kutoka Chuo Kikuu cha Addis Ababa Ethiopia aliambia jarida hilo kwamba dalili za kutokea kwa bahari zimeanza kuonekana katika maeneo ya jangwani ya Ethiopia, eneo la Afar ambalo pia linahusisha baadhi ya maeneo ya Eritrea na Djibouti.
Mwaka 2005, alisema tayari nyufa nyingi zimeanza kutokea na ardhi imebonyea kwa hadi mira 100.
Ufa huo ulianza kuonekana wiki moja iliyopita baada ya mvua kubwa kunyesha na barabara ya Mai Mahiu kwenda Narok ikakatika eneo lenye ufa huo.
Awali, wengi waliamini ufa huo uliotokea Jumanne wiki iliyopita eneo la Karima ambalo linapatikana kilomita sita kutoka mji wa Mai Mahiu ulitokana na mvua kubwa.
Ufa huo uliokuwa umeikata barabara hiyo ulikuwa umeenea umbali wa mita 700.
Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Barabara Kenya (KeNHA) wakishirikiana na mkandarasi kutoka China anayejenga reli ya kisasa, walifika eneo hilo na kuziba ufa.
Baada ya uchunguzi, ilibainika kwamba ulitokana na shughuli ya kijiolojia chini ya ardhi ambayo ilihusisha mvutano wa vipande vikubwa vya ardhi.
Siku chache baadaye Jumapili, ufa huo uliendelea kupanuka na kuathiri barabara hiyo tena jambo lililosababisha magari yenye kubeba mizigo mizito kutoweza kupita.
Aidha, ufa huo ulianza kuathiri nyumba za wakazi.
"Mkandarasi na kundi la wahandisi wamewekwa hapo kwa sasa na watasalia kuendelea kufuatilia yanayojiri kutokana na shughuli za kivolkano ambazo zilisababisha ufa huo," alisema naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa KeNHA Charles Njogu baada ya ukarabati huo mara ya kwanza.
Bw Adede amesema hatua ya kuziba ufa huo kwa sasa itasaidia kwa muda mfupi tu.
Ufa huo umepitia katika baadhi ya nyumba na mashamba ya watu.
Mmoja wa walioathirika ni Eliud Njoroge, 77, ambaye ameambia BBC kwamba ameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20.
Anasema amelazimika kuibomoa nyumba yake na sasa analazimika kuishi kama 'mkimbizi' kwa jirani yake.
Baadhi ya maeneo, ufa huo una upana wa mita 20 na kina cha hadi futi 50.
Wataalamu wametahadharisha kwamba nyufa zaidi zinaweza kuendelea kuonekana katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa.
Viongozi wa eneo lililoathirika wamewahimiza wakazi wanaoishi karibu na maeneo yaliyotokea ufa huo kuhama, lakini baadhi kama Bw Njoroge hawawezi kuhamia mbali.
0 Post a Comment:
Post a Comment