Wanasiasa, Watumishi wa Umma Kupigwa Marufuku TLS

Mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zimewagonganisha viongozi wake na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) baada ya kudaiwa kuongezwa masharti yanayowanyima fursa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi ndani ya chama hicho.

Kanuni hizo zimechapishwa juzi katika Gazeti la Serikali (GN) namba 116, jambo ambalo limekifanya chama hicho kuitisha kikao cha dharura kujadili mabadiliko hayo kwa maelezo kuwa hakikuyapitisha katika kikao cha baraza la uongozi.

Kipengele hicho kinacholalamikiwa na TLS ni cha (8)(e) kinachoeleza masharti ya mwanachama anayetaka kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kuwa asiwe mtumishi wa umma, mbunge, diwani au kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa.

Pia, Rais wa TLS, Tundu Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu amedai kuwa saini yake imeghushiwa katika kanuni hizo inayoonyesha alisaini Februari 9.

Jana, Makamu Mwenyekiti wa TLS, Godwin Ngwilimi alisema, “Hiki kipengele hakikupitishwa katika kanuni za kikao cha baraza la uongozi ambazo zilikwenda kwa AG, lakini zimerudi kikiwa kimeongezwa, kwa nini aliweka muulize AG.”

Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu kuzungumzia madai hayo, AG Dk Adelardus Kilangi alijibu kwa kifupi “sorry (samahani) sizungumzi katika magazeti.”

Kuhusu hatua ambazo TLS itachukua kutokana na utata huo, Ngwilimi alisema, “Kwanza tayari ishakuwa katika gazeti la Serikali, mimi siwezi kutoa uamuzi wangu, tumeitisha kikao cha dharura cha kujadili suala hilo. Hatujajua AG ametumia mamlaka gani kuweka hayo mabadiliko.”

Kuhusu madai ya Lissu kwamba saini yake imeghushiwa, Ngwilimi alisema saini hiyo haijaghushiwa kwani iliyotumika ni saini ya kielektroniki ambayo baada ya kikao cha baraza la uongozi kumaliza kupitisha kanuni, mmoja wa watumishi wa TLS aliiweka.

“Hata Lissu analijua hilo, lakini kwa kuwa kipengele hicho kimeongezwa ndiyo anasema imeghushiwa lakini kama isingeongezwa kipengele hicho sidhani kama angeongea, lakini hili nalo la saini ni moja ya mambo tutakayojadili kwenye kikao hicho cha dharura.”

Kwa upande wake, Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa Chadema alisema, “Vita ya mwaka jana inaendelea...”

“Wanajua hawaniwezi kwenye sanduku la kura za mawakili... Mimi sijashiriki kikao au shughuli yoyote ya TLS tangu wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ waliponipiga risasi nyingi mwaka jana,” alisema Lissu.

“Nitasaini vipi kanuni za uchaguzi zilizopitishwa na kikao ambacho sikukiendesha wala kukihudhuria?”

Ngwilimi alipoelezwa kuhusu Lissu kupinga saini yake kutumika wakati hakuwapo kwenye kikao alisema “Hilo sasa siwezi kulisemea lakini muulize yeye ni mjumbe wa baraza la uongozi, alipowauliza walimjibu nini.”

Hata hivyo, Lissu alipoulizwa swali hilo alisema “Walifanya hivyo kwa idhini ya nani? Mimi sikuwepo kwenye kikao husika, sikushiriki kwenye kufanya maamuzi haya na sikusaini au kutoa idhini ya sahihi yangu kutumika kwenye maazimio ya kikao husika.

“Sahihi yangu imetumika huko nyuma kwenye kikao gani ambacho sikukihudhuria? Hakuna, kwa kadri ninavyofahamu hii ni hoja ya ajabu kabisa. Maana yake ni kwamba wanaweza kutumia sahihi yangu ya kielektroniki kutolea pesa benki na ikawa sawa tu.”

Download App YETU hapa⬇⬇



Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: