Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amesema hata kama wamekuwa wakinyamaza, haina maana kwamba wapinzani hawaumizwi na mambo wanayofanyiwa bungeni.
Bulaya alisema hayo jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo bungeni mjini Dodoma.
“Tukitoka mnasema, tukikaa mnatunyanyasa. Mnataka tufanye nini? Leo mko madarakani, kesho hamko madarakani. Kwa nini mnatuchagulia cha kusema?” alihoji Bulaya.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo kufuatia Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Zungu kuzuia baadhi ya maneno yaliyomhusisha aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane kuagiza yafutwe katika kitabu cha hotuba ya upinzani.
Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa suala la mahali alipo halijawahi kuwa wazi, hivyo kuibua sintofahamu nchini.
Baada ya kauli hizo, Zungu ambaye jana alionekana dhahiri kumvumilia msemaji wa upinzani wa wizara hiyo,
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema, “kiti hiki hakiongozwi na Serikali na hakina mrengo wa Serikali. Nimeshatoa ruling na ruling zangu hazihojiwi humu, bali kwa kufuata kanuni ya tano. Unaandika barua kwa katibu wa Bunge naye anaiwasilisha kwa Spika.”
0 Post a Comment:
Post a Comment