Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amekosolewa ndani na nje ya nchi yake kuhusu mpango wa kuunda bunge litakaloandika katiba mpya.
Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za Amerika, OAS, Luiz Almagro amesema hatua hiyo haikubaliki na ni kinyume cha katiba.
Marekani imesema kuwa bunge la katiba ni njama tu za kumfanya Maduro aendelee kubaki madarakani huku Brazil nayo ikisema kuwa huo ni mpango wa kufanya mapinduzi.
Bunge la Congress linalodhibitiwa na upinzani limepiga kura kukataa bunge jipya la katiba, likisema kuwa halitaundwa bila wao kuridhia.
Wakati hayo yakijiri, katika hatua nyingine waandamanaji kwa mara nyingine wamejitokeza barabarani na kusababisha misururu mirefu ya magari.
Wakati rais Maduro akiona kwamba hatua hii ni ya kuwavunja nguvu wapinzani ambao amewashutumu kutaka kumpindua, hasimu wake Henrique Capriles amesema hayo ni maneno ya serikali iliyoshindwa ambayo inataka kukwepa kuitisha uchaguzi.
Amesema maandamano yataendelea.
0 Post a Comment:
Post a Comment