KENYA:UCHAGUZI MPYA UTAFANYIKA OKTOBA 26

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM
27 Sep 2017

 Uchaguzi mpya wa urais Kenya ulioitishwa baada ya maamuzi ya Mahakama ya Juu sasa utafanywa Oktoba 26, siku tano kabla ya kipindi cha siku 60 kilichowekwa na mahakama hiyo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), Wafula Chebukati ametangaza uamuzi huo umechukuliwa ili kuhakikisha tume hiyo inajitayarisha vilivyo kutokana na hukumu kamili na Mahakama ya Katiba iliyotolewa Jumatano iliyopita.
Tume ya Uchaguzi imeibadilisha tarehe iliyoiweka awali, Oktoba 17, na imeiomba Serikali iipatie Sh12.2 za Kenya ili kuendesha uchaguzi huo baada ya matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi, kubatilishwa.
Katika uamuzi wake juu ya madai yaliowasilishwa na mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga, Mahakama iligundua uchaguzi huo haukuwa huru na haki, pia ulikuwa kinyume na Katiba na sheria.
Rais Uhuru Kenyatta ameilaumu Mahakama hiyo kwa kutoa uamuzi uliomzuia kuapishwa kuwa rais kwa muhula wa pili na akatishia kwamba mamlaka ya majaji yatachunguzwa upya baada ya yeye kushinda uchaguzi wa marudio.
Jaji mmoja katika jopo la walioisikiliza kesi hiyo, aliulinganisha mwenendo mzima wa uchaguzi uliopita kuwa kama gari la daladala lisilojali sheria za barabarani.
Mahakama ilisema uchaguzi wa Agosti 8 ulikuwa haujahakikiwa, na kwamba IEBC ilishindwa, ilidharau na kukataa kuendesha uchaguzi mzuri na ulio wazi, kama ilivyotakiwa na Katiba.
Kwa hivyo kulikuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kuyabatilisha matokeo. Moja kati ya mifano muhimu: kukosekana kuandikwa matokeo ndani ya fomu za karatasi kutoka karibu vituo 11,000 kati ya zaidi ya vituo vya uchaguzi 44,000 nchini kote, na kuingizwa kwa njia ya kielektroniki katika kompyuta ya Tume. Jambo hilo halijafanywa.
Zile fomu zilizotumwa, kwa mfano, hazijawa na mhuri rasmi, nyingine zilikuwa hazijatiwa saini sawa na nyingine hazijawa na nambari au alama rasmi, hivyo kuweko wasiwasi kama fomu hizo ni za halali.
Tume ya Uchaguzi, licha ya kuamriwa na Mahakama ya Katiba, ilikataa kuachia mfumo wake wa kielektroniki kuchunguzwa, kwa hivyo wengi wa majaji walilazimika kuukubali mtazamo wa upinzani kwamba mfumo wa kompyuta wa Tume ya IEBC uliingiliwa na kuchakachuliwa.
Japokuwa Mahakama ilisema haijaweza kupata ushahidi wa moja kwa moja ni maofisa gani wakuu wa IEBC waliochakachua na kusababisha dosari zilizotajwa, hata hivyo, upinzani umesisitiza kwamba hautaweza kushiriki katika uchaguzi ujao pindi watu wanaoshukiwa kuhusika na uchafuzi uliopita hawatawekwa kando katika kusimamia uchaguzi ujao.
Jambo hilo linapingwa na chama tawala cha Jubilee cha Rais Kenyatta, kikisema Tume ya Uchaguzi ni huru na isiingiliwe katika shughuli zake za kuteua watu gani wa kusimamia uchaguzi na taratibu zitakazofuatwa katika mchuano huo.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2007 Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanywa Durban nchini Afrika Kusini ulipitisha itifaki ili iingizwe ndani ya Azimio la Hati ya Afrika ya Haki za Binadamu na ikatajwa kwamba ni muhimu kuhakikisha kuna utawala bora kupitia njia ya wananchi kushiriki.
Ilisisitizwa kwamba chaguzi ndio msingi wa Serikali yeyote inayowakilisha wananchi na ni ufunguo wa mwenendo wa kidemokrasi. Ilitajwa kwamba chaguzi lazima ziendeshwe kwa njia iliyo huru na ya haki, chini ya Katiba za kidemokrasi, chini ya mfumo wa kugawa madaraka baina ya mihimili mitatu ya utawala, Serikali, Bunge na Mahakama – hasa kuhakikisha uhuru wa Mahakama.
Itifaki hiyo ilisema lazima ihakikishwe kwamba chaguzi si tu lazima ziwe huru na za haki, lakini lazima zionekane dhahiri kuwa ni huru na za haki mbele ya walimwengu.
Kuweko tume huru siku hizi kunaonekana kuwa ni hatua muhimu ya kujenga tabia ya uhuru na kutopendelea upande wowote pamoja na kupata vilevile imani ya wapiga kura na ya vyama vya kisiasa vinavyoshiriki katika chaguzi zenyewe.
Swali ni kama IEBC itaweza kufanya uchaguzi safi, ikijulikana kwamba Mahakama ya Juu ya Kenya imesema haitasita kuchukua tena msimamo kama iliouchukua pindi makosa yaliyofanyika hapo kabla yatarejewa. Kikatiba, kwa vyovyote vile, tarehe ya mwisho ya kufanywa uchaguzi mpya ni Oktoba 30. Kama Tume ya Uchaguzi itaweza kumaliza matayarisho yote hadi siku ya uchaguzi Oktoba 26 ni suala la kusubiri. Lakini, endapo uchaguzi kwa namna yeyote vile hautaweza kufanywa hadi Oktoba 30, basi Kenya itaingia katika mzozo wa kikatiba.
Rais wa sasa atabakia madarakani hadi pale rais mpya atakapochaguliwa na kuapishwa. Lakini, kuna wataalamu wengine wanaohoji kwamba pindi siku 60 za rais wa sasa za kujishikiza zikimalizika na hakuna rais mpya aliyechaguliwa na kuapishwa, basi spika wa bunge atakamata wadhifa huo wa kuwa kaimu rais hadi pale rais mpya atakapochaguliwa na kuapishwa.
Na ikiwa spika hatakamata nafasi hiyo ya kujishikiza, basi atafuata Jaji Mkuu. Na hapo kitakuwako kiroja cha mambo kwani itakuwa ni zamu ya David Maraga, Jaji Mkuu aliyebatilisha kuchaguliwa kwa rais wa sasa kukamata nafasi hiyo.
Hiyo ndio maana Uhuru Kenyatta anadai kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ya Katiba wa Septemba Mosi yalikuwa mapinduzi yaliofanywa na Mahakama kuupindua uamuzi wa wananchi wa Agosti 8.
Jumanne iliyopita Jaji Maraga mbele ya waandishi wa habari alilaumu juu ya vitisho vinavyoelekezwa kwa Mahakama, tangu pale ulipotangazwa uamuzi wa kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8.
Vitisho hivyo vilianza pale Rais Kenyatta alipoiita “Mahakama ya Maraga na wakora wenzake.” na kutishia kuisafisha pale atakapochaguliwa tena kuwa rais.
Tamko hilo liliwachochea wafuasi wa Kenyatta kwenda barabarani na pia kuongeza sumu kupitia mitandao ya kijamii. Maraga alitaja vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Mahakama na kusema kwamba mkuu wa polisi, Joseph Boinnet, hajawapa ulinzi wa kutosha.
Kwa mshangao aliongeza kusema: “Tuko tayari kulipia gharama ya juu kabisa ili kuilinda katiba ya nchi.”
Wakati wa joto hili la kisiasa, Kenyatta na Odinga inabidi wajiandae na kampeni ngumu ya uchaguzi, kuranda tena kila kona ya nchi kuomba kura.
Duru ijayo ya uchaguzi huenda ikawa chafu zaidi kuliko ile iliyopita, hofu ya kutokea machafuko bado ipo. Kinyume na uchaguzi wa Agosti, huu hautaingiza kugombea ubunge, useneta, ugavana, uwakilishi wa wanawake au kuwa mjumbe wa baraza la mkoa (County).
Hivyo vishindo huenda vikapungua, lakini kuna hatari kwamba nguvu zote na mori wote ukaelekezwa katika mabishano ya watu wawili, Kenyatta na Odinga.
Hali hiyo ina hatari zake, hasa uhasama wa kikabila, jambo ambalo si geni katika siasa za Kenya.
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: