WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako amefanya ziara ya kushtukiza katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kilichopo Gongolamboto, Dar es Salaam na kubaini madudu.
Miongoni mwa madudu hayo ni pamoja na kuwepo watumishi wa serikali ambao pamoja na kufanya kazi za utumishi wa umma, wana ajira za kudumu chuoni hapo.
Chuo hicho pia kimeajiri walimu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, Kenya, Nigeria, Ireland, India na Cuba ambao hawana vibali vya kuishi nchini huku wengine wakiwa na vibali vya matembezi lakini wameajiriwa.
Kuwepo kwa walimu wa shule za sekondari katika chuo hicho lakini kwenye malipo wanaonekana ni walimu wa Chuo Kikuu huku chuo hicho kutokuwa na Mkuu wa chuo anayetambulika na kubadilika mara kwa mara jambo ambalo limewafanya wanafunzi wa chuo hicho kutotambua nani ni Mkuu wao wa Chuo.
Pia utawala wa chuo hicho kutoa taarifa za uongo kuhusu watumishi wao ikiwemo kuwaingiza walimu wakidai ni wanafunzi lakini wapo katika orodha ya malipo pamoja na kuonesha idadi kubwa ya walimu wa Tanzania lakini kwenye malipo wanaonekana ni watumishi wa kawaida kama madereva na wahudumu.
Dosari nyingine ni udanganyifu wa sifa za wanataaluma wao huku wengine wakiwa na Shahada za Uzamivu (PHD) zilizofutwa na serikali ya Uganda, wafanyakazi kuwa na Viwango vya Juu vya Ufaulu (GPA) ambavyo si halali pamoja na kuwapa watu Uprofesa wakati hawana sifa hizo.
Mbali na madudu hayo ziara hiyo pia imewakamata walimu 32 kutoka nchi mbalimbali waliokuwa wanakimbia kwa kuruka kuta za chuo hicho baada ya kuona msafara wa Waziri na kukabiliwa maofisa Uhamiaji ambao walikuwa wamezingira kuta hizo na kuchukuliwa kwa hatua zaidi.
Ndalichako alisema ameamua kufanya ziara hiyo baada ya watendaji wa chuo hicho kufika ofisi kwake kwa madai kuwa wanaonewa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ikiwemo kunyimwa kufanya udahili huku wakiwa wamekamilika kila idara.
“Wamekuwa wakija kunitembelea kwa madai kuwa wanaonewa na TCU ikiwemo kunyimwa udahili mimi nikaona ni vyema niwatume watu wangu kuja kufuatilia lakini baada ya kuniletea ripoti nimebaini bado mna shida kubwa kama chuo lazima tuzungumze pamoja na kupata majibu,”alisema.
Akizungumzia uwepo wa watumishi wa umma kuajiriwa katika chuo hicho huku wakiendelea kufanya kazi serikalini Ndalichako alisema, kanuni ya utumishi wa umma 2009 inasema kuwa mtumishi wa umma hapaswi kufanya kazi sehemu mbili kama mwajiriwa.
“Hapa nimebaini uwepo wa watumishi wa umma wengine wakiwemo chini ya Wizara yangu kama huyu Dk Amos Nsanganzelu ambaye yupo DIT (Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Saalam).
“Pia yupo Dk Geodfrey Towo ambaye yupo MUHAS (Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili) na Bupe Mwabenga ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Babro Johanson. Sasa hawa siwataki katika Wizara yangu wabaki huku huku haiwezekani ukatumikia mabwana wawili wamepoteza uaminifu na serikali.
“Leo nimetoa Sh 50,000 kwa mwanafunzi ambaye anamjua Mkuu wa chuo lakini hakuna hata mmoja anayemfahamu mkuu wa chuo zaidi ya Rais wa wanafunzi hii inawiana na hii kuwa uongozi haudumu leo yupo huyu kesho huyu,”alisema.
0 Post a Comment:
Post a Comment