Serikali yatenga fedha kumaliza migogoro sugu ya ardhi kwenye maeneo ya jeshi

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM=>

Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeahidi kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wananchi na jeshi kwa kulipa fidia wananchi ambao ardhi zao zimechukuliwa na Jeshi bila kulipwa kwa muda mrefu.

Ahadi hiyo imetolewa jana Februari 8, 2018 Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi wakati akijibu swali la Mbunge wa Dimani Juma Ally Juma lililohoji mpango wa serikali katika kutatua mgogoro wa muda kati ya Jeshi na Wananchi wa eneo la Kisakasaka, visiwani Zanzibar.

Dkt. Mwinyi alisema wizara yake imetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaostahili hasa wale waliochukuliwa maeneo yao na Jeshi pasipo kulipwa fidia.

“Kambi nyingi ambazo zina migogoro ya ardhi, iko ya aina nyingi kuna migogoro ambayo Jeshi limechukua ardhi  ya wananchi hawajalipa fidia, wananchi wamevamia maeneo ya kambi na kadhalika, tumeweka fedha kwenye bajeti ya wizara ili kwenye maeneo ambayo fidia zinahitajika tuweze kulipa fidia, ili kumaliza migogoro, mwaka wa bajeti haujaisha na ni mategemeo yetu fedha zikipatikana tuanze kulipa fidia kwa wanaostahili kulipwa fidia maana wengine wapo wamevamia hawastahili kulipwa fidia,” alisema.

Kuhusu mgogoro wa Kisakasaka, alisema serikali inautambua mgogoro huo uliokuwepo tangu mwaka 1979, na kwamba kilichokwamisha utatuzi wa mgogoro huo ni ukosefu fedha jambo ambalo wizara yake imetenga fedha ili kuleta suluhisho la kudumu kwenye mgogoro huo.

“Wizara ya ulinzi inatambua uwepo wa mgogoro wa ardhi kati ya jeshi na wananchi katika eneo la kisakasaka, katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huu, makao makuu ya jeshi imeridhia kurekebisha mpaka wa kambi ya kisakasaka ili kuwaachia wananchi eneo la mgogoro na hivyo kuleta suluhisho la kudumu kwenye mgogoro huo. Zoezi hilo halijafanyika kutokana na ufinyu wa bajeti, hata hivyo katika mwaka huu wa fedha wa mwaka 2017/18 tunategemea kutekeleza zoezi hilo,” alisema.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewasihi wananchi wa Kisakasaka kuwa wastahimilivu wakati serikali inachukua hatua stahiki ili kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutokea, endapo wataendelea na shughuli za kilimo na mifugo katika eneo hilo. 
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: