Wanachama 400 na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Bagara na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngarenaro Mjini Babati mkoani Manyara, Nicodemus Tlaghasi (Chadema) aliyejiuzulu hivi karibuni wamekabidhiwa kadi za CCM.
Katibu wa Uenezi, Siasa, Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga alikabidhi kadi ya CCM kwa wanachama hao wapya na diwani huyo aliyejiuzulu jana mjini Babati.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi kadi hizo mpya, Lubinga amewataka wanachama hao 400 na Tlaghasi, kuwa waaminifu kwenye chama hicho.
Amesema CCM ya hivi sasa inaendana na kasi kulingana na dunia ilivyo, hivyo wajiandae kwenda mwendo kasi ili kufikia maendeleo chanya.
Amesema inapotajwa CCM mpya na Tanzania mpya maana yake ni kuwa Watanzania wa sasa mahitaji yao si ya juzi na jana hivyo viongozi waliopatiwa dhamana ya kuongoza inawabidi watimize wajibu wao ipasavyo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya CCM, Tlaghasi amesema amechoka kuishi maisha ya wasiwasi yasiyo na amani, ambayo alikuwa anayaishi wakati akiwa kiongozi wa jamii kupitia Chadema.
Amesema alikuwa anaishi maisha ya kuvizia ili asionekane na viongozi wa Chadema pindi akitaka kutimiziwa mahitaji ya jamii kwenye Serikali kwani alikuwa anaonekana kama msaliti.
"Ili kuonana na kiongozi wa serikali ilinipasa kuvizia, lengo likiwa nitimize mahitaji ya wapiga kura wangu, nikajiuliza nateseka hivi kwa ajili ya nini?" Alihoji Tlaghasi.
Amesema dhamira yake ikamtuma kuachana na Chadema na kujiunga na CCM ili aungane na Rais John Magufuli na mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti katika kuwatumikia wananchi.
0 Post a Comment:
Post a Comment