Jeshi la Polisi lafungua jalada kubaini ukweli kuhusu mwenyekiti TSNP



Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limeeleza kuwa limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama Mwenyekiti wa  Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Omari Nondo alikuwa ametekwa au la ili liweze kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire akiongea na waandishi wa habari ameeleza kuwa bado uchunguzi dhidi ya tukio hilo unaendelea ili waweze kubaini kama ni kweli ametekwa na kuwakamata wahusika kwa ajili ya kuwachukulia hatua zaidi za kisheria.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa alimefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa, na kama kweli alikuwa ametekwa tunaahidi kwamba sisi jeshi la polisi tukiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake,” amesema Kamanda Bwire.

Kamanda Bwire ameongeza kuwa pamoja na kufanya uchunguzi, jeshi hilo linapeleleza zaidi ili kujiridhisha kama taarifa iliyotolewa ni ya uongo kwa nia ovu ya kuhamasisha wanafunzi nchini kuleta uvunjifu wa amani, na wakibaini hilo watamchukulia hatua kali za kisheria.

“Aidha tunaendelea kuchunguza kama ametoa tarifa za uongo kwa nia ovu, kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini. tutamshughulikia kama wahalifu wengine,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda bwire amesema kuwa Abdul anaonekana kuwa na afya njema na hana majeraha yoyote kuashiria kuwa alipigwa au kuteswa.

“Kwa sasa anaonekana hali yake ni nzuri, hana majeraha yoyote, hajapigwa ni mzima wa afya njema. hivyo basi Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kupitia maeneo yote aliyopitia ili tuweze kujua nini kilichomsibu,” alisema Kamanda.

Vile vile aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi wakati wa uchunguzi dhidi ya tukio hilo ili waweze kubaini kilichotokea na wahusika waweze kufikishwa mahakamani.

Abdul Nondo (24) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka wa tatu kitivo cha Siasa na Utawala, alisemekeana kupotea katika mazingira ya kutatanisha siku ya Jumanne majira ya kati ya saa 5 na 6 usiku jijini Dar es Salaam na kupatikana jana Jumatano akiwa Mkoani Iringa.

Download App YETU hapa⬇⬇


Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: