Mkuu wa Mkoa apingana na agizo la Waziri Kigwangala

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametengua agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliyewapa miezi tisa wananchi wa Kijiji cha Kimotorok kuondoka katika maeneo wanayoishi wakidaiwa kuvamia Hifadhi ya Tarangire wilayani Simanjiro.

Akizungumza na wanakijiji hao juzi, Mnyeti alisema hakuna atakayekwenda kuwafukuza na kama hilo lipo, yeye ndiye atawaambia wanafukuzwa au la, hivyo wawe na amani.

Mnyeti alisema ofisi ya mkoa inajiandaa kutuma wataalamu kwenda kupima eneo hilo ili kutatua mgogoro.

Februari 25, Waziri Kigwangalla aliwapa wananchi wa kijiji hicho, vitongoji vya Massas na Loon’benek miezi tisa wawe wamehama kwa kuwa wamevamia eneo la Hifadhi ya Tarangire.

Baadaye alitoa ufafanuzi akisema kabla ya kuondoka, Serikali itawalipa fidia na watatafutiwa maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kujengewa zahanati nje ya hifadhi kutokana na iliyokuwapo kuwa ndani.

Dk Kigwangalla alipotafutwa jana kuzungumzia kauli ya Mnyeti alisema, “Sijapata taarifa rasmi kwa maandishi. Siwezi kufanyia kazi taarifa za kwenye mitandao. Nitasubiri barua kama itakuja. Hata hivyo, sina hakika kama mkuu wa mkoa anaweza kusema hivyo.”

Mkuu wa mkoa Mnyeti alitoa kauli baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi wa Kimotorok alipokuwa akienda kwenye mkutano wa kuwapokea wanachama zaidi ya 3,000 wa CCM kutoka vyama vingine.

Wananchi wa kijiji hicho walimuomba mkuu wa mkoa kuingilia kati suala hilo kwani watu wa hifadhi wanataka kuwapora ardhi yao bila hata kuwashirikisha katika jambo lolote wanalofanya, ikiwamo kuweka alama  ndani ya ardhi ya kijiji hicho ambacho kina hati miliki tangu mwaka 1970.

Akijibu hoja za wananchi, Mnyeti aliomba apewe siku 10 awe amefanya utaratibu wa kupeleka wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao wako katikati ya wananchi na hifadhi hivyo hawatapendelea upande wowote.

“Sasa chagueni kamati ndogo au Serikali ya kijiji watakaokwenda na wataalamu kukagua alama za mipaka. Watapitia mipaka yote kujua ramani maana hifadhi nayo ina umuhimu wake, hivyo muwe tayari kukubaliana na majibu yatakayosomwa na mtaalamu baada ya ukaguzi maana hata ofisi ya ardhi mkoa haijui utekelezaji wa uwekaji alama hizo,” alisema Mnyeti.

Alisema, “Lakini pia inawezekana mko sahihi maana tunajua hawa watu wa hifadhi mara nyingi wao wanataka kusogeza tu eneo, kila siku wanataka eneo liongezeke, leo anaweza akaja akaishia hapa kesho akija anaishia hapa, sasa tunaleta mtu ambaye yuko katikati ya hifadhi na wananchi na atapima kuleta ukweli.”


Download App YETU hapa⬇⬇


Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: