Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Odinga wakutana, waahidi kuwaunganisha Wakenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo Raila Odinga katika afisi yake Jumba la Harambee, Nairobi.
Wawili hao wamekubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa rasmi karibuni
Balozi Martin Kimani ataongoza kuundwa kwa mpango huo upande wa Rais Kenyatta naye mshauri wa Bw Odinga Paul Mwangi atawakilisha Bw Odinga, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Bw Kenyatta na Bw Odinga baada ya mkutano huo.
Mkutano huo umefanyika muda mfupi kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.
Marekani imekuwa ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo baada ya uchaguzi uliojaa utata mwaka jana.
Bw Odinga alitangulia kuhutubia taifa moja kwa moja na baadaye Bw Kenyatta akatoa hotuba yake.
Bw Kenyatta amesema wamekubaliana na Bw Odinga kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.
Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."
"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze."
"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna araia anayehisi ametengwa."
"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu."
"Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya."
Bw Odinga amesema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.
"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Bw Odinga.
"Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa lililofeli."
Bw Tillerson atawasili nchini Kenya baadaye leoHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionBw Tillerson atawasili nchini Kenya baadaye leo
Bw Odinga mesema wamekubaliana kufanikisha mabadiliko yatakayofanikiwa mageuzi nchini humo, na pia kukomesha kulaumiana.
Amewataka Wakenya waunge mkono mpango wa viongozi hao wawili.
"Tumesafiri mbali sana kiasi kwamba hatuwezi kurudi tena bandarini. Isitoshe, hatuwezi kufika tunakoenda bila kufanya mabadiliko la sivyo tutazama baharini," amesema Bw Odinga.
"Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee pamoja," amesema Bw Odinga.
  • 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
  • 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
  • 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
  • 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya
  • 9 Machi, Bw Kenyatta akutana na Bw Odinga katika afisi ya rais Jumba la Harambee, wawili hao waahidi kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.


Download App YETU hapa⬇⬇


Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: