Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto, Unicef limesema kuwa kuna mafanikio makubwa ya kupungua kwa ndoa za utotoni duniani.
Shirika hilo la Unicef limekadiria kuwa ndoa za utotoni zipatazo milioni 25 zimeweza kuzuiliwa katika muongo iliyopita.
Kwa sasa ni msichana mmoja kati ya watano anaolewa chini ya miaka 18 tofauti na miongo iliyopita ambapo ilikuwa msichana mmoja anaolewa kati ya wanne.
Shirika hilo la watoto limesema Kusini mwa nchi za bara la Asia wamejitahidi zaidi katika kupunguza ndoa za utotoni.
Anju Malhotra, mshauri wa masuala ya jinsia kutoka Unicef anasema haya ni mabadiliko mazuri katika maisha ya wasichana wote duniani hivyo upunguaji wa vitendo hivyo hata kwa kiwango kidogo ni habari njema ingawa bado kuna safari ndefu ya kutokomeza ndoa hizo za utotoni.
Hali ikoje nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine ya karibu?
Kwa mujibu wa takwimu za Unicef za kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.
Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 31.
Nchini Kenya, ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa nguvu kubwa ya kutokomeza tatizo hili la ndoa za utotoni ilihamia Afrika,ambapo jitihada zaidi zilihitajika ili kupunguza tatizo hilo.
Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Kwa sasa ripoti inaelezwa kuwa ndoa moja ya utotoni inafungwa kati ya ndoa tatu katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara wakati miongo iliyopita ilikuwa ndoa utotoni moja kati ya ndoa tano za utotoni.
Hata hivyo jitihada za matokeo ya mabadiliko haya ni kutokana na kampeni nyingi zilizofanywa duniani ingawa bado changamoto zipo katika kufikia lengo hilo.
Uhamasisho zaidi unahitajika Tanzania:
Hivi karibuni shirika la kiraia la Equity Now lilifanya utafiti nchini Tanzania ambapo bado sheria ya ndoa ya nchini humo haijaweka wazi juu la suala la kutetea ndoa za utotoni.
Shirika hilo lilifanya utafiti mkoani Kilimanjaro na kubaini kuwa tatizo kubwa linatokana na watoto kushindwa kulindwa na jamiii kwa ujumla na vilevile wahusika wakuu wa ndoa hizi za utotoni ni jamaa wa karibu na ndugu katika familia.
Bi Florence Machio mhamasishaji wa haki za watoto kutoka Equity Now anasema, yeye alifanya utafiti huo kwa kufanya mazungumzo na watoto wenye umri kati ya 11 na 18 kutoka shule mbalimbali na lengo lilikuwa ni kuondoa fikra ya mila na desturi za kiafrrika ambazo, watoto wenyewe hawapewi nafasi ya kueleza matatizo yao wakati wao ndio walengwa.
Na Florence anasema maswali mengi waliuliza kwa kuandika na inaonekana kuwa hawana ueleo mkubwa juu ya matatizo wanayokumbana nayo na namna ya kutafutia suluhisho, kwa mfano kuna mtoto aliuliza je ,kama wazazi wangu wamenilazimisha kuolewa nikienda kutoa taarifa polisi na yeye ataenda wapi na hatima ya maisha yake yatakuwaje?
Anasema mara nyingi watunga sera au wanaopigania haki za watoto hawawaulizwi watoto wanasemaje juu ya changamoto zinazowakabili.
Nichodemas Shauri kutoka mtandao wa elimu Tanzania, yeye anasema taarifa ni tatizo na miongoni mwa masuala muhimu ambayo ni jukumu la walimu kuwafundishwa masuala ya kijamii na stadi za maisha ili watoto waweze kukabiliana na changamoto ambazo wanazokutana nazo za mimba ya utotoni.
Watoto wana imani kubwa kutoka kwa walimu zaidi ya wazazi wao ,hivyo kuna umuhimu kwa mfumo wa elimu kuweka jitihada zaidi hata katika mafunzo ya walimu ili kuwawezesha watoto kuwa na ueleo kwa kuwa waathirika wakubwa ni watoto wa kike ambao sio wao wa kulaumiwa ila mfumo mzima unaleta athari katika kulinda usalama wa ukuaji wa watoto.
Aidha viongozi duniani wamejizatiti katika malengo ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030.
0 Post a Comment:
Post a Comment