Mwanamke mzaliwa wa India amefanikiwa kuupanda Mlima Everest hadi kileleni katika kipindi cha chini ya wiki moja ambayo huenda ikawa rekodi mpya kwa wanawake.
Anshu Jamsenpa, 37, ambaye ni mama wa watoto wawili, alifika kileleni tarehe 16 Mei na akarejea tena 21 Mei,
Rekodi ya sasa ya dunia ya Guinness ya kuupanda mlima huo mara mbili kwa kasi zaidi ni ya siku saba kwa wanawake.
Habari za mafanikio hayo ya Jamsenpa zimetangazwa huku kukiwa na habari za tanzia, baada ya wapanda mlima zaidi ya watatu kufariki wakiukwea mlima huo mwishoni mwa wiki.
Mpanda milima kutoka Australia alifariki akikwea mlima huo kutoka upande wa Tibet naye raia wa Slovakia na Mmarekani wakafariki upande wa Nepal.
Maafisa wa uokoaji wameshindwa kumfikia mpanda milima wa nne, ambaye anatoka India, na ambaye alitoweka muda mfupi baada ya kufika kileleni.
Mamia ya wapanda milima wanatumai kufika kilele cha mlima huo mrefu zaidi duniani kabla ya mvua za vuli kuanza kunyesha mwezi ujao.
Hii ni mara ya pili kwa Bi Jamsenpa, anayetoka jimbo la Arunachal Pradesh, kujaribu kupanda Mlima Everest mara mbili.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2011, ambapo alipanda baada ya siku 10.
Sasa anahitajika kuwasiliana na maafisa wa Guinness World Records rekodi yake itambuliwe baada yake kuthibitishwa rasmi na wizara ya utalii ya Nepal.
Rekodi ya sasa iliwekwa na mwanamke kutoka Nepal, Chhurim Sherpa mwaka 2012.
Bi Jamsenpa alikuwa pia ameukwea mlima huo 2013.
0 Post a Comment:
Post a Comment