Ikiwa leo ni Kumbukumbu ya Kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine aliyefariki dunia Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari, eneo la Dakawa nje Kidogo ya Mji wa Morogoro, Rais Dkt. John Magufuli amefunguka na kueleza alivyomfahamu kiongozi huyo enzi za uhai wake na mchango wake katika Taifa letu.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Magufuli amesema;
“Katika siku kama ya leo tarehe 12 Aprili 1984 nikiwa Mpwapwa JKT nikitumikia jeshi langu “Oparesheni Nguvukazi” tukatangaziwa kifo cha marehemu Edward Moringe Sokoine, ilikuwa siku ya majonzi shujaa huyu niliyemjua na kumshabikia ikawa siku yake ya mwisho.
“Wakati tunapoazimisha siku kama hii ya kifo chake, watanzania tuige mfano wake kwani alikuwa msema kweli, asiyeogopa, mpiga vita rushwa,ufisadi, unyonyaji,mzalendo wa kweli na aliyechukia rasilimali za watanzania kuibwa.
“Marehem Sokoine hatasahaulika katika historia ya Tanzania, ni wito wangu kwa watanzania tumuige na kumuishi. Ni rai yangu pia tumuenzi kwa kujenga umoja wetu , kupiga vita rushwa na kuchapa kazi . Mungu aiweke roho ya marehemu Edward Moringe Sokoine mahala pema peponi,” amesema Magufuli.
0 Post a Comment:
Post a Comment