Kamusi Kuu ya Kiswahili yazinduliwa Tanzania


20 Juni 2017

Kamusi kuu Tanzania
Waziri Mkuu wa Tanzania , Kassim Majaliwa akionyesha Kamumusi Kuu ya Kiswahili baada ya kuizindua kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Juni 19, 2017. Kulia ni Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu. Kushoto ni Balozi wa Kiswahili Afrika, Mama Salma Kikwete. Wapili kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali yake inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa taifa na katika kulinda umoja wa kitaifa.
Ametoa kauli hiyo alipozungumza na wabunge, viongozi wa Serikali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
"Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tunaithamini na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa," amesema.
Kamusi kuu TanzaniaWaziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu nakala ya Kamusi Kuu ya Kiswahili baada ya kuzindua kamusi hiyo kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma


Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake amesema uzinduzi wa kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.
Majaliwa amempongeza Rais John Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake kutoka nje.
"Hata alipokuwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili," amesema.
Waziri Mkuu , amewasihi wazazi wahakikishe watoto wao wanapata kamusi hiyo kama moja ya nyenzo zao za kujifunza lugha ya Kiswahili."Ninashauri makundi mengine kama vile waheshimiwa wabunge, wanahabari, wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa mawasiliano wa kwenye ofisi zetu, muone umuhimu wa kununua kamusi hii ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu," amesema.
Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Dk Seleman Sewangi amesema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na kukamilika mwaka 2015 na toleo la kwanza lilichapishwa.Amesema kamusi hiyo imekusanya maneno mengi makuu (vidahizo) kuliko kamusi zilizotangulia na kwamba ya sasa ina maneno 45,500.

Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: