Je, ni kweli mafuta ya taa huondoa mihemko ya ngono?


20 Mei 2017



 Baadhi ya shule za sekondari za bweni nchini zinatuhumiwa kutumia kiasi kidogo cha mafuta ya taa katika chakula cha wanafunzi kwa lengo la kuwapunguzia mihemko ya ngono.
Sekondari kadhaa zikiwamo za Serikali na seminari zimetajwa kutumia mbinu hiyo, ambayo baadhi ya madaktari wa afya waliohojiwa na gazeti hili wamesema kisayansi mbinu hiyo haisaidii kupunguza tatizo hilo.
Imeelezwa kuwa mbinu ya kutumia mafuta ya taa kwenye chakula inatokana na wanafunzi wengi kujihusisha na ngono, hivyo kujiweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya zinaa, kama Ukimwi na mimba.
Mmoja wa watu aliyewahi kukumbwa na mbinu hiyo aliyeomba jina lake lisitiriwe na ambaye alisoma seminari moja mkoani Kagera, alisema kwa miaka minne ya masomo alikumbana na milo kadhaa iliyonuka mafuta ya taa.
“Nakumbuka mara kadhaa tuliwashambulia wapishi kwa maneno makali, lakini hakuna sababu ya maana waliyowahi kutujibu. Mara zote walitujibu kuwa ni bahati mbaya,” alisema.
“Tena chakula cha mafuta ya taa tulikuwa tunapewa siku moja kila tunapokuwa na ratiba au taarifa ya kutembelewa na shule ya wasichana kwa ajili ya mazoezi ya kitaaluma. Jambo hilo lilitutesa. Hadi tunahitimu hatukuwahi kupata suluhisho,” alisema.
Theresia Marko akizungumza na gazeti moja hapa nchini alisema amesoma shule ya Serikali iliyopo mkoani Pwani na kwamba alikuwa akihisi chakula kuwekewa mafuta ya taa.
“Awali hatukubaini kinachoendelea kwenye mlo, lakini baada ya udadisi ndipo tulibaini kwamba hayawekwi kwa bahati mbaya. Eti yanasaidia kupunguza ashiki. Mara nyingi tulikumbana na hali hiyo tunapotoka likizo au tunapokaribia kwenda likizo,” alisema.
“Chakula kikiwa na mafuta ya taa ni kibaya. Yaani unalazimika kula kwa sababu njaa inauma, ingawa nakumbuka kuna siku tulisusa na kuamua kulala na njaa maana haikuwa harufu pekee bali tulisikia ladha halisi ya mafuta kwenye ndimi zetu.”
Mpishi wa shule mojawapo ya jijini hapa, Juma Bushir alisema kuna mpishi mwenzake aliwahi kumlalamika jinsi alivyoshambuliwa kwa maneno na wanafunzi wa shule aliyokuwa akifanya kazi baada ya wanafunzi hao kukerwa na harufu ya mafuta ya taa.
“Aliniambia mwenzako siku yangu imekuwa ngumu kwa jinsi wanafunzi walivyokasirika na kunung’unika jinsi chakula kinavyonuka mafuta ya taa. Yeye aliyasikia yakinuka kwenye chakula,” alisema.
“Rafiki yangu huyo aliniambia kwamba baada ya kuwasiliana na uongozi wa shule alijibiwa kwamba mafuta hayo hayana madhara. Pia yanasaidia kuwapunguzia ashiki ya kufanya ngono wanafunzi ili wawe makini na masomo.”
Alisema hata yeye hakuwa anajua ukweli kuhusu mafuta ya taa kupunguza ashiki, na hata kwenye shule aliyokuwa akifanyia kazi hakuwahi kusikia hilo.
Mbali na shule za sekondali nchini, Desemba 2, 2014 wanasayansi wanne wa Kenya walichapisha ripoti ya utafiti kuhusu mafuta ya taa kupunguza mihemko ya ngono katika jarida la Sayansi la Elsevier.
Kilichowasukuma wanasayansi hao kufanya utafiti ni kuenea kwa taarifa kwamba shule nyingi za bweni katika nchi za Afrika Mashariki na nyinginezo, zinatumia mafuta ya taa kwenye chakula cha wanafunzi kuwapunguzia hamu ya ngono.
Ripoti ya wanasayansi hao ilisema walipofanya utafiti kwa kutumia panya waligundua kundi lililopewa mafuta kidogo liliongeza ashiki kwa asilimia 66 na lile lililopewa mengi liliongeza kwa asilimia 75.
Maana yake mafuta ya taa yaliongeza ashiki badala ya kupunguza, na kwa upande wa sumu hakukuwa na madhara makubwa.
Pia, ripoti hiyo ilibainisha kwamba utafiti wa wanasayansi hao kwa baadhi ya shule za Kenya uligundua wanafunzi waliwekewa mafuta hayo kwenye chakula, lakini yalichochea zaidi ongezeko la mimba, usaliti kwa uongozi wa shule na vurugu.
Daktari wa magonjwa ya binadamu nchini, Gunini Kamba alionyesha kushtushwa na mbinu hiyo wakati alipozungumza na gazeti hili. Alisema ingawa hajaona au kufanya utafiti, ni wazi kuna madhara kwa binadamu kula mafuta ya taa.
“Mafuta ya taa hayafai kuliwa, hii siyo mbinu salama kwa afya za hao vijana, bali wanaweza kusaidiwa kwa kukutanishwa kwenye michezo, burudani ikiwemo muziki wakiwa jinsi mbili tofauti wakazungumza na kufurahi pamoja,” alisema Dk Kamba.
“Mafuta ya taa ni distillate (mabaki) ya mafuta ya ghafi. Harufu yake inakera na husababisha baadhi ya watu kulewa,” alisema.
“Nasisitiza msaada wa karibu kwa kijana anapovuka umri ni kumjengea uelewa wa masuala ya kujamiiana na kumjengea hali ya kujiamini na kufurahi kwa kukutana na kujumuika katika michezo au burudani ilimradi pawe mahali salama,” alisema Dk Kamba.
Mtaalamu wa afya ya akili, Dk John Chikomo naye alishtushwa na mbinu hiyo, akieleza kwa kifupi kuwa hajawahi kusikia kama mafuta ya taa yanaweza kuwa msaada wa kudhibiti mhemko.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee, Meja Robert Kessy alisema mbinu ambayo wamekuwa wakiitumia shuleni hapo kuwapunguzia mhemko wa ngono wanafunzi ni pamoja na kuwafanyisha mazoezi.
“Tunachofanya sisi ni kuwafanyisha mazoezi na shuguli nyingine zinazohusu masomo yao. Lakini pia tumekuwa na utaratibu wa kuwaandalia matamasha na kuwajumuhisha na wengine wanafurahi pamoja,” alisema Meja Kessy.
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: