RAILA ODINGA NA KALONZO WAONDOLEWA ULINZI

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM
26 Sep 2017

Kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga amelishutumu Jeshi la Polisi kwa kupanga vitisho baada ya walinzi wake na wa mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka kurejeshwa makao makuu.
Walinzi wa Odinga na wale wa Musyoka waliondolewa jana jioni.
Maofisa hao wa polisi walirejeshwa makao makuu ya polisi katika mkesha wa maandamano makubwa yaliyokuwa yamepangwa na muungano wa Nasa kwenda makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ili kung’oa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu Ezra Chiloba kwa madai kuwa ndiye alivuruga uchaguzi wa Agosti 8.
Maandamano hayo yamefanyika kama ilivyopangwa leo katika miji ya Nairobi na Kisumu lakini Odinga, Musyoka na maofisa wengine wa juu wa Nasa hawakushiriki.
Odinga amesema hatua ya serikali kumnyima haki ya ulinzi ilikuwa sehemu ya mradi mkubwa wa kutaka kuwadhuru viongozi wa upinzani.
Odinga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Capitol Hill alisema kwa sheria yeye anastahili kuwekewa ulinzi na serikali.
"Hakuna aliyenijulisha kuhusu kuondolewa kwao. Nilipoamka nikakuta wamerejeshwa,” amesema Odinga.

Waandamanaji wapigwa
Katika hatua nyingine, polisi wamelazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya Jubilee na muungano wa upinzani wa Nasa baada ya kuzua vurugu katika ofisi za IEBC zilizoko jengo la Anniversary Towers.
Wafuasi wa Nasa waliokuwa wakiimba nyimbo “Chiloba lazima ang’oke” walikabiliwa na wafuasi wa Jubilee waliokuwa wakiimba “Tunataka amani”. Makundi yote mawili yalitimua mbio baada ya polisi wa kuzuia ghasia kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.
Huku wakikohoa na wakitafuta mahali salama, wote walikimbia kukwepa kukamatwa.
Maandamano hayo yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu wa Nasa Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi kwenye makao makuu ya IEBC lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.
Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Katika mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.
Walimshutumu Chiloba na kikundi chake kwa kufanya njama za kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu ambao matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalifutwa na Mahakama ya Juu.
Waandamanaji waliokuwa wamebeba matawi ya miti, mabango huku wakipiga yowe na honi za pikipiki walianzia barabara ya Obote wakaenda mtaa wa Oginga Odinga kabla ya kuchukua Barabara Kuu ya Kenyatta na baadaye Mtaa wa Ang’awa katikati ya jiji.
 TUFUATE FACEBOOK:ZAKACHEKA.HABARI
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: