VIKAO kazi vya kujadili ili kuwapanga upya madaktari kwa uwiano vyaanza Dar es salaam

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM=>
VIKAO kazi vya kujadili ili kuwapanga upya madaktari kwa uwiano, utakaoleta tija kwa nchi nzima na kuwahamishia madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwenda katika Kampasi ya hospitali hiyo ya Mloganzila, vimeanza kufanyika jijini Dar es Salaam.
 Vikao hivyo vimeanza kufanywa na watendaji wa juu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kama utekelezaji wa haraka wa ushauri uliotolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli.
Rais Magufuli alitoa ushauri huo wakati akizindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kampasi ya Mloganzila iliyopo wilayani Kisarawe, mkoani Pwani wiki iliyopita.
Katika ushauri wake, Rais Magufuli alielezea nia yake ya kuona Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inalifanyia kazi suala hilo la kuwapanga vizuri zaidi madaktari katika mikoa yote nchini ili wananchi wapate huduma bora zaidi za afya.
Kulifanyika kikao cha watendaji wa wizara hiyo Dar es Salaam jana ili kujadili suala hilo kwa kina na hata alipoulizwa kuhusu hilo kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya alithibitisha.
Ulisubisya alisema kuwa agizo la Rais la kuwahamishia madaktari na wataalamu wa afya katika Hospitali ya Mloganzila na pia kuangalia namna ya kuwapanga upya madaktari, limeanza kufanyiwa kazi.
Pasipo kueleza kwa undani, Dk Ulisubisya alisema jana kuwa alikuwa anaongoza kikao, kilichokuwa kinajadili suala hilo na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu baada ya kukamilika kwa kazi hiyo. Ushauri wa Rais kuhusu madaktari Katika maelezo yake, Rais Magufuli alisema kuwa asilimia 60 ya madaktari bingwa wako jijini Dar es Salaam na asilimia 40 iliyobaki ya madaktari ndiyo wako mikoani, hatua ambayo haileti uwiano sahihi wa kuwahudumia wagonjwa.
Rais aliitoa mfano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa ina vitanda 1,600 na jumla ya madaktari 532, wakiwemo madaktari bingwa, madaktari wanafunzi na madaktari wahadhiri.
Kwa takwimu hizo, Rais alisema daktari mmoja wa Muhimbili anahudumia vitanda vitatu, ikilinganishwa na Hospitali ya Mkoa wa Tabora ambako daktari mmoja anahudumia wagonjwa 208,329, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012. Rais Magufuli aliishauri Wizara ya Afya kuwahamishia Hospitali ya Mloganzila watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Magonjwa ya Ndani (Internal Medicine).
Kwa mujibu wa Rais, Kitengo cha Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Muhimbili kina uniti 8, hivyo kama wahudumu wote wa kitengo hicho na wagonjwa wakihamishiwa Mloganzila, hospitali hiyo itakuwa imepata jumla ya madaktari 73 na 40 kati yao ni madaktari bingwa, wauguzi wahudumu 169 na wagonjwa zaidi ya 250.
Rais alisema kuwa Hospitali ya Mloganzila ina uhitaji wa watumishi wa afya 950, lakini pia kuna vitanda 571 ambavyo havina wagonjwa. Aliwataka watumishi wa afya kuwa wazalendo na kuwa tayari kufanya kazi mahali popote watakapopangiwa. Jambo jingine ambalo Rais aliiagiza Wizara ya Afya ni kuzihamisha hospitali za mikoa kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kuwa chini ya Wizara ya Afya.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa mahitaji ya wahudumu wa afya nchini ni 184,901, lakini waliopo ni 89,842, hivyo kuna upungufu wa watumishi wa afya 95,059, na vibali vya ajira vilivyotolewa ni 3,410
•Tuma habari picha na video za matukio mbalimbali WhatsApp kwa ,0625966236
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: