China kushiriki ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa

ZAKACHEKA.BLOGSPOT.COM=>
BALOZI wa China nchini, Wang Ke, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushawishi taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Exim ya nchini humo, kushiriki ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa mradi huo.
Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za Marekani bilioni 7.6 hadi kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kukidhi masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na taasisi nyingine, zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu.
“Mradi huu ni muhimu na wa kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa kuona mradihuo unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria na kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara kwa kuwa shehena kubwa ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo,” alisema.
Aidha, Balozi Ke alisema kuwa nchi yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu za ndani kati yake na Tanzania ili mradi wa reli ya Mamlaka ya Tanzania na Zambia (TAZARA), uanze ili kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia pamoja na nchi za Maziwa Makuu.
Balozi Ke alitumia fursa hiyo, kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za umma, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.
Akizungumza baada ya mazungumzo na mgeni wake, Waziri Mpango alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) ili China kupitia taasisi zake iweze kujenga sehemu ya mradi huo.
“Tayari mradi umeanza kujengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwa hiyo kujitokeza kwa China kutaka kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia kukamilisha mradi huo muhimu kwa haraka na kwa wakati,” alisema Dk Mpango.
Alisema pia kuwa China imeonesha nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa Dodoma kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa kupanga miji, ambapo nchi hiyo imeonesha nia ya kujenga miundombinu ya elimu, barabara, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka pamoja na majengo ya kisasa.
Kuhusu biashara, Dk Mpango alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia Tanzania kukuza kiwango cha biashara, ambapo takwimu zilizoko zinaonesha kuwa urari wa biashara kati ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikinunua bidhaa nyingi kutoka nchini humo kuliko inavyouza bidhaa na huduma zake.
“Mwaka 2016 Tanzania iliuza China bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 460 wakati China iliuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa karibu mara tano ya kile tulichowauzia,” alisema Dk Mpango.
Ili kuvutia sekta ya utalii, Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya ndege wa moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii wengi kutoka nchini humo na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya Usafiri wa Anga iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na hivyo kufanikisha jambo hilo.
“China imeandaa maonesho makubwa ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali mwezi Novemba, 2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja na Bodi ya Utalii nchini wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutumia nafasi hiyo kujitangaza,” alisisitiza Dk Mpango.
Aidha, alieleza kuwa Balozi Wang Ke, alisema kuwa nchi yake itashiriki katika ujenzi wa miradi ya bandari ili kukuza masuala ya usafiri kwa kuboresha bandari za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Waziri huyo wa Fedha alitoa wito kwa wawekezaji kutoka China na nchi nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki, ambacho Tanzania inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
•Tuma habari picha na video za matukio mbalimbali WhatsApp kwa 0625966236
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: