Serikali imesema imeanza mchakato wa kuajiri watumishi 52,436 wanaohitajika katika kada mbalimbali nchini.
Hayo yalielezwa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alipowasilisha hotuba yake kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Alisema uhakiki wa mahitaji ya rasilimali watu katika utumishi umma ikiwamo mikoa yote, umefanyika kupitia Mfumo wa HCMIS na kubaini idadi hiyo ya mahitaji ya watumishi wa kada mbalimbali.
"Serikali imeanza mchakato wa kuajiri watumishi hao kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele na kuimarisha kada zenye upungufu mkubwa," alisema.
Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Newala, alibainisha kuwa kada ya afya ina upungufu wa watumishi 14,102, elimu 16,516, kilimo 1,487, mifugo 1,171 na uvuvi 320.
Aliongeza kuwa polisi kuna upungufu wa watumishi 2,566, magereza 750, uhamiaji 1,500, zimamoto 1,177, hospitali za mashirika ya kidini na hiari 174 na wengineo 12,673.
Mkuchika alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha, usimamizi wa ajira za watumishi wa umma umefanyika kwa waajiri wote ambapo watumishi wapya 15,000 wameajiriwa, wakiwamo jumla ya walimu 4,348 wa masomo ya sayansi na watumishi 3,152 wa kada ya afya ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti.
"Maofisa utumishi 1,595 wamechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufungiwa dhamana ya kuingia katika mfumo wa HCMIS, kufikishwa mahakamani na wengine kesi zao zipo Takukuru," alisema Mkuchika.
Download App Yetu hapa chini, Bonyeza picha:-
0 Post a Comment:
Post a Comment