29 Mei 2017
Jared Kushner ni mmoja wa wasaidizi wakuu wa Donald Trump
Kushner ni mumewe binti wa kwanza wa Trump, Ivanka
Rais wa Marekani Donald Trump amejitokeza kumtetea mkwe wake Jared Kushner, baada ya taarifa kutokea kwamba Kushner, ambaye kwa sasa ni mshauri wake katika ikulu ya White House, alijaribu kuanzisha njia ya kisiri ya mawasiliano na maafisa wa Urusi.
Kwenye taarifa ambayo imekabidhiwa gazeti la New York Times, Bw Trump amemsifu Kushner na kusema kwamba anafanya "kazi nzuri".
Hata hivyo, hajazungumzia moja kwa moja tuhuma zinazomkabili mwanamume huyo ambaye ni mumewe binti wa kwanza wa Bw Trump, Ivanka.
Taarifa zinadai kwamba Bw Kushner alijadiliana na balozi wa Urusi kuhusu uwezekano wa kuanzisha njia ya kisiri ya kuwasiliana na maafisa wa Urusi mwezi Desemba.
Magazeti ya New York Times na Washington Post yanasema alitaka kutumia huduma za Urusi kukwepa mawasiliano hayo kusikika na majasusi ya Marekania akiwasiliana na maafisa wa Moscow.
Anadaiwa kufanya hivyo kabla ya Bw Trump kuapishwa kuwa rais, na kwa hivyo wakati huo alikuwa tu raia wa kawaida.
Tuhuma hizo zimeibuka baada ya Bw Kushner kudaiwa kuwa miongoni mwa wanaochunguzwa na FBI kuhusu tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.
Taarifa nchini Marekani zinasema maafisa wana habari muhimu, lakini kwamba si lazima iwe kwamba hilo lilikuwa kosa la jinai.
Bw Trump, ambaye inadaiwa alikutana na mawakili White House siku ya Jumapili, ambaye bado anamuunga mkono Bw Kushner, ambaye kwa sasa ni mshauri wa ngazi ya juu White House.
"Jared anafanyia nchi hii kazi nzuri sana. Nina imani naye kikamilifu," alisema kupitia taarifa kwa New York Times.
"Anaheshimiwa na karibu kila mtu na anafanyia kazi mipango ambayo itasaidia nchi yetu kuokoa mabilioni ya dola. Kadhalika, na labda muhimu zaidi, yeye ni mtu mwema."
Matamshi ya Bw Trump yametokea baada ya maafisa wakuu wa utawala wake kupuuzilia mbali tuhuma hizo, bila kusema iwapo zilikuwa za kweli.
Waziri wa usalama wa ndani John Kelly aliambia ABC News Jumapili kwamba ni kawaida kuwa na njia za kisiri za kuwasiliana na mataifa yenye ushawishi.
Mshauri wa usalama wa taifa wa Bw Trump HR McMaster pia alisema "tuna njia za faragha za kuwasiliana na mataifa kadha."
0 Post a Comment:
Post a Comment