Mabilionea wengi walio na umri mdogo duniani, ambao hawakurithi mali kutoka kwa wazazi wao, walijipatia utajiri wao kupitia uwekezaji katika sekta ya teknolojia, kwa mujibu wa jarida la Forbes.
Kwenye orodha ya mabilionea waliopo duniani, Forbes wanasema kati ya mabilionea 2,208 ni 63 pekee ambao ni wa chini ya miaka 40.
Idadi hiyo hata hivyo imeongezeka kutoka 56 mwaka 2017.
Kati ya matajiri wa umri mdogo waliopo kwa sasa duniani, 34 ndio waliojitafutia utajiri wao ambapo 26 wamejizolea utajiri kupitia uwekezaji katika sekta ya teknolojia.
Baadhi wamepata utajiri wao kupitia kuunda mitandao yao ya kijamii na huduma za biashara kwa kutumia simu na mtandao.
Wengine wameunda kampuni za kuwawezesha watu kutumia bidhaa na huduma kwa pamoja, mfano kukodisha nyumba kwa kipindi ambacho mtu amesafiri.
Mabilionea wote wa chini ya miaka 40 ambao walijizolea utajiri wao kupitia kuwekeza ni wanaume.
Wanawake wote 16 mabilionea wa chini ya miaka 40 walirithi utajiri wao.
Kwa jumla, mabilionea wote wa chini ya miaka 40 wanamiliki mali ya thamani ya $265 bilioni, idadi ambayo imeongezeka kutoka $208 bilioni.
Mabilionea wa umri mdogo zaidi duniani
Kwa mwaka wa tatu mtawalia, mabilionea wa umri mdogo zaidi ni wanawake wawili kutoka Norway - Alexandra na Katharina Andresen walio na miaka 21 na 22 mtawalia.
Baba yao Johan H. Andersen aliwapa umiliki wa kampuni ya familia kwa jina Ferd mwaka 2007. Wawili hao wana utajiri wa dola $1.4 bilioni kila mmoja.
Katharina Andresen aligonga vichwa vya habari Aprili 2007 aliposimamishwa na polisi Aprili 2017 akiendesha gari lake la kifahari aina ya Audi Q3 karibu na kituo kimoja cha kutelezea kwenye barafu akiwa mlevi.
Alikuwa amepitisha kiwango kilichoruhusiwa mara tatu. Majaji walimpiga faini ya $32,000 na leseni yake ya kuendesha magari ikasimamishwa kwa miezi 13.
Bilionea wa umri mdogo zaidi ambaye amejitafutia utajiri wake ni John Collison, 27, ambaye ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Stripe.
Alianzisha kampuni hiyo kwa pamoja na nduguye Patrick Collison, 29, ambaye pia yumo kwenye orodha ya mabilionea wa umri mdogo zaidi. Kampuni ya wawili hao Novemba 2016 ilikadiriwa kuwa na thamani ya dola 9.2 bilioni. Wote wawili utajiri mali yao ni $1 bilioni kila mmoja.
John Collison ni mdogo kidogo wa umri kwa mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Snap inayomiliki mtandao wa Snapchat ambaye pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo Evan Spiegel. Utajiri wa Evan ni $4.1 bilioni. Mwaka uliopita, aliongoza mpango wa kuuboresha mtandao wa kijamii wa kampuni hiyo wa Snapchat.
'Zuckerberg wa Urusi'
Mtu mgeni katika orodha ya mabilionea hawa ni Pavel Durov ambaye amekuwa akifahamika kama Mark Zuckerberg wa Urusi.
Yeye ndiye mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa pili kwa ukubwa Urusi, mtandao wa Vkontakte.
Wote wawili wana miaka 33. Aliuanzisha mtandao huo akiwa na miaka 22 mwaka 2007.
Mtandao wake wa kijamii una watumiaji zaidi ya 400 milioni.
Yeye pia ndiye mmiliki mkubwa wa mtandao wa Telegram ambao unatumiwa na watu zaidi ya 100 milioni duniani.
Lynsi Snyder ni tajiri mwingine ambaye kwa sasa ana miaka 35 na utajiri wa $1.2 bilioni.
Alirithi sehemu ya biashara ya hoteli za familia yake ya In-N-Out nchini Marekani. Babu na bibi yake
Harry na Esther Snyder walianzisha biashara hiyo mwaka 1948.
Bilionea tajiri zaidi wa umri mdogo
Bilionea tajiri zaidi miongoni mwa walio na chini ya miaka 40 ni Mark Zuckerberg ambaye anawazidi wengine pakubwa.
Utajiri wake ni $71 bilioni.
Bilionea wa pili tajiri zaidi wa umri mdogo ni Yang Huiyan ambaye ni mrithi katika kampuni kubwa ya uwekezaji katika nyumba na ardhi yenye makao yake China.
Ana miaka 36 na utajiri wake unakadiriwa kuwa $21.9 bilioni. Yang humiliki asilimia 57% ya hisa katika kampuni ya Country Garden Holdings ambao ni urithi kutoka kwa babake Yeung Kwok Keung alioupokea 2007.
Watu kumi matajiri zaidi duniani wa chini ya miaka 40
10. Mark Zuckerberg, 33,
Utajiri wake: $71 bilioni
Marekani, Facebook
9. Dustin Moskovitz, 33
Utajiri wake: $14 bilioni
Marekani,Facebook
8. Julio Mario Domingo III, 32
Utajiri wake: $2.2 bilioni
Marekani, Pombe
7. Ginia Rinehart, 31
Utajiri wake: $1.3 bilioni
Australia, Madini
6. Patrick Collins, 29,
Utajiri wake: $1 bilioni
Ireland, Stripe
5. Bobby Murphy, 29
Utajiri wake: $4.2 bilioni
Marekani, Snapchat
4. John collison, 27
Utajiri wake: 1 bilioni
Ireland ,Stripe
3. Evan Spiegel, 27
Utajiri wake: $ 4.1 bilioni
Marekani, Snapchat
2. Katharina Andresen, 22
Utajiri wake: $1.4 bilioni
Norway, uwekezaji
1. Alexandra Andresen,21
Utajiri wake: $1.4 bilioni
Norway, uwekezaji
0 Post a Comment:
Post a Comment