Marais katika bara la Afrika wanavyojiandalia anguko


Marais katika bara la Afrika wanavyojiandalia anguko

 
WEDNESDAY, APRIL 5, 2017

By Joster Mwangulumbi, Mwananchi
Ni vioja. Viongozi au watawala wajeuri au wenye kiburi huwa wanapigwa upofu wasione wanaelekea kwenye anguko lao. Katika Afrika wapo wengi ndiyo maana hata Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Binadamu (ICC) inaliangazia bara hili.
Mtawala mmoja anapoanguka na kuondolewa kwa aibu, kutupwa jela na kulazimishwa kuishi uhamishoni, wengine hawatumii hali hiyo kama fundisho ili wabadili njia yasiwakute mambo hayo.
Mmoja wa watawala hao ni aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh ambaye baada ya kulewa madaraka alijiongezea jina la Babili Mansa ambalo kwa kabila lake la Mandika lina maana ya Mtengenezaji Mkuu Daraja au Mshindi wa Mito. Kwa hiyo, akawa anaitwa Mtukufu Sheikh Profesa Alhaji Dokta Yahya AJJ Jammeh Babili Mansa kabla ya kuliacha mwaka 2014.
Mwaka 2011 aliviambia vyombo vya habari kwamba atatawala kwa miaka bilioni moja iwapo Mungu atamruhusu. Ulevi huo ulimfanya ashindwe kutumia fursa ya kujifunza juu ya yaliyowakuta Charles Taylor wa Liberia au Zine El Abidine Ben Ali wa Tunisia au Hosni Mubarak wa Misri au Muammar Gadaffi wa Libya lakini hakubadilika.
Pamoja na kujinasibu huko kuwa ana baraka zote za Mungu, sasa “ameikimbia” nchi yake anaishi uhamishoni Guinea ya Ikweta.
Upofu kifikra aliopata Jammeh hadi anaanguka ndiyo waliopigwa wengi, lakini bado mtawala huyu jeuri au dikteta anatoka, huyu anaibuka, hawaishi.
Labda tofauti na miaka ya 1960 hadi 1990 wengi wakiingia kwa mtutu wa bunduki, watawala jeuri wa leo wanaingia kwa sanduku la kura, lakini hujifunga vitambaa usoni ili waendeleze udhalimu. 
       Watawala wenye kiburi huona ushujaa wa watu wanaoandamana kupinga maovu ya Serikali ni uchochezi na hujibu kwa ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu – kuwakamata mara kwa mara, kuwatia mahabusu, kuwafungulia kesi za kisiasa – ilimuradi tu kujenga uhalali wa kuendelea kukalia ofisi ambazo huenda hawakushinda kihalali kutokana na ukiukwaji wa taratibu na vitisho.
Rais Jammeh
Jammeh alitwaa madaraka kwa mapinduzi ya umwagaji damu mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka 29 kwa kumwondoa Dawda Kairaba Jawara, rais aliyeiongoza nchi kupata uhuru mwaka 1962. Hakujifunza kutokana na kilichomkuta Blaise Compaore wa Burkina Fasso ambaye mwaka 1986 alimwondoa kwa kumuua Thomas Sankara lakini naye aliondolewa kwa nguvu ya umma mwaka 2014.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu Desemba Mosi, 2016, Serikali ya Jammeh iliwatia ndani viongozi wengi wa upinzani kwa madai ya kukiuka sheria ya mikusanyiko ya watu.
Katika moja ya mikutano yake, Jammeh alidai wapinzani ni “watu wanafiki” wanaotegemea nchi za Magharibi. “Nitamsujudu Allah na kumheshimu mama. Kamwe sitawavumilia wapinzani wavuruge amani ya nchi,” aliapa Jammeh kwa kauli sawa na aliyoitoa Gaddafi akiwaita wapinzani wake “mende”.
Labda alipoona watu wako kimya alidhani anapendwa Gambia nzima. Lakini siku ilipowadia alishuhudia yakitokea ambayo hakuyatarajia, watu walewale walioonekana kondoo, wasio na sauti walizungumza kupitia sanduku la kura kwamba hawamtaki.
Bila kutarajia Jammeh, ambaye alikuwa kiongozi wa tisa katika orodha ya waliokaa muda mrefu madarakani barani Afrika baada ya kuongoza kwa miaka 22, alishindwa vibaya na akakiri kushindwa kwa mgombea ambaye hakuwa maarufu aliyekuwa anaungwa mkono na upinzani, Adama Barrow.
Siku tisa baadaye alikataa matokeo akilalamikia “kasoro zisizokubalika” na kisha alitangaza kuyafuta hadi ufanyike uchaguzi mwingine. Lahaula, Jammeh hakuwa amejua kuwa ‘kondoo’ walisimamia haki yao akashurutishwa kuachia madaraka.
Mazingira yakawa magumu, hawezi kuishi tena Gambia, akalazimika kwenda kuishi ugenini huku akichota kutoka hazina Dola za Marekani 11 milioni pamoja na magari ya kifahari. Jammeh alikwenda uhamishoni huku akipishana na waliokuwa wametoroka nchi kwa sababu yake, wao sasa wanarejea kwa amani.
Jammeh hakuona kama amekaa miaka mingi kwani wapo wengine hadi leo barani Afrika kama Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea aliyekaa madarakani kwa miaka 37, Robert Mugabe wa Zimbabwe (miaka 36), Paul Biya wa Cameroon (miaka 33), Yoweri Museveni wa Uganda (miaka 31), Omar Bashir wa Sudan (miaka 27) na Idris Derby wa Chad (miaka 26).
Jammeh ameingia katika orodha ya viongozi wengine mashuhuri waliolazimishwa kutoka ikulu na kuachia madaraka.
Charles Taylor
Rais huyo wa zamani wa Liberia hivi sasa yuko gerezani Uingereza baada ya kutiwa hatiani na mahakama iliyokuwa inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuunga mkono waasi waliotenda unyama Sierra Leone.
Kitabu kiitwacho “Almasi za Damu: Kufuatilia Njia ya Mauti ya Mawe yenye thamani zaidi duniani” kilichoandikwa na mwanahabari wa Marekani, Greg Campbell ni moja ya vitabu vinavyoelezea kwa kina unyama aliotekeleza Taylor.
Aliiba karibu dola za Marekani 100 milioni za Liberia alipokuwa madarakani, kwa mujibu wa rekodi za Serikali kutokana na uchunguzi wa UN ambazo alizitumia kununua majumba, magari na silaha kwa ajili ya vita hivyo.
Baada ya shinikizo kubwa la jumuiya ya kimataifa, Taylor ambaye aliingia madarakani mwaka 1990 baada ya kumpindua na kumuua Samuel Doe kisha kukata sehemu zake za siri na kutembeza mitaani, alijiuzulu mwaka 2003, akakabidhi ikulu kwa Rais Moses Blah na akaomba hifadhi ya kisiasa Nigeria ambako alikamatwa alipokuwa anajaribu kutoroka. Polisi wa kimataifa (Interpol) walitoa hati ya kumkaamata.
Kesi yake ilianza mwaka 2007 na alitiwa hatiani mwaka 2012 kutokana na mashtaka 11 baadhi yakiwa mauaji, ubakaji, kuwatumia watoto kama waasi katika vita vya Sierra Leone na ugaidi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1991 na 2002 vilivyosababisha vifo vya watu 50,000.
Marais wengine
Vuguvugu la mapinduzi ya Kiarabu yaliyoibuka mwaka 2011 yaliwang’oa madarakani Rais wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali; Rais wa Misri, Hosni Mubarak; na Kiongozi wa Libya, Muammar Gadaffi.
Ben Ali aliingia madarakani mwaka 1987 baada ya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu yaliyomtupa nje Rais Habib Bourguiba aliyeongoza tangu uhuru mwaka 1956. Ben Ali alikimbilia Saudi Arabia, lakini alihukumiwa jela miaka 35.
Aidha, Mubarak aliyejiuzulu baada ya maandamano ya siku 30, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa uhalifu uliotendeka kipindi hicho cha maandamano. Mahakama ilimfutia mashtaka mwezi uliopita na hivi karibuni aliachiwa huru.
Pia, Gadaffi mbabe wa Afrika aliyeingia madarakani mwaka 1969 aliogopwa, kuheshimika na kuabudiwa. Vuguvugu lilipoanza Februari 2011 aliapa kuwasaka waasi chini kwa chini, chumba kwa chumba, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa na kuwaua kama mende, lakini alitimuliwa Agosti na akauawa.
Viongozi wengine walioondolewa madarakani ni Marc Ravalomanana wa Madagascar (2009) tena na DJ Andry Rajoelina; Laurent Gbagbo wa Ivory Coast (2011); na Amadou Toumani Toure wa Mali (2012); Jenerali Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika Kati (2013); na Blaise Compaore wa Burkina Fasso (2014) aliyeingia madarakani mwaka 1987 kwa kumuua rafiki yake Rais Thomas Sankara in 1987.
Faida zao
Watawala wa kiimla hushangiliwa wanapoingia madarakani kwa sababu huendesha mambo chapchap, mchakato huchukua muda mfupi kufikia uamuzi kwa sababu hutegemea kauli ya mtu mmoja tu. Pia, huwa hakuna nafasi kubwa kwa rushwa na ufisadi na kiwango cha uhalifu huwa kidogo.
Hasara zao
Baadaye huchukiwa kwa sababu uwepo wa viongozi wa kiimla kuna hasara kubwa. Uongozi huwa mbaya unaoweza hata kudumaza taifa; hakuna uhuru wa kiuchumi, uhuru wa watu hubanwa, hakuna uhuru wa kisiasa. Mara nyingi hekima na busara hukosekana na hutengeneza maadui wengi.
Chini ya utawala wa kiimla, Bunge linaweza kuwapo lakini lisiwe na nguvu, katiba inaweza kuwepo lakini baadhi ya ibara zikazimwa. Kwa kuwa uongozi hujenga hofu hali ya siasa na uchumi katika taifa havitabiliki.
Watawala hawa wanapoona wameharibu hutafuta mbinu za kusalia madarakani muda mrefu kama Joseph Kabila wa DR Congo na Pierre Nkuruzinza wa Burundi. Wengine hubadili huanza kubadili ibara zilizoweka ukomo wa mihula na hupiga marufuku vyama vya siasa japokuwa katiba zinaruhusu.     
 
Share on Google Plus

ABOUT BLOGGER INJILI HALISI MINISTRY

Hi! I am Zachary John Bequeker, from Mwanza Tanzania, East Africa.I'm a blogger of ZAKACHEKA NEWS LINE And ZAKKACHEKA INJILI.Contact me +255 625966236 / +255 758590489 or mail on zacharybequeker@gmail.com . Thanks!!!

0 Post a Comment: